Habari

Mirengo ya BBI yaanza kumtia Ruto kiwewe

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

KAMPENI za kurekebisha Katiba chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI) zinaendelea kuchukua mkondo wa siasa za 2022, hali inayoonekana kumtia wasiwasi Naibu Rais William Ruto.

Kufikia sasa, kuna mirengo mitatu ambayo imeibuka ikiwa na misimamo tofauti kuhusu mswada wa kura ya maamuzi ambao tayari umepata zaidi ya saini milioni tano za wapigakura.

Mrengo wa kwanza ni wa viongozi wanaounga mkono BBI, wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Chini ya mrengo huo, kuna vigogo wengine wa kisiasa kama vile Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Seneta wa Baringo Gideon Moi (Kanu) na mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Katika upande wa pili, kuna kikundi ambacho kinapinga kabisa marekebisho ya Katiba kwa msingi kuwa marekebisho yoyote wakati huu yatavuruga Katiba iliyopitishwa 2010 ambayo haijatekelezwa kikamilifu.

Kikundi hiki kinaongozwa na wanasiasa kama vile Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana, Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, kwa ushirikiano na wanaharakati kama vile Boniface Mwangi, Dkt David Ndii na aliyekuwa Jaji Mkuu, Dkt Willy Mutunga.

Mrengo wa tatu ni ule wa Dkt William Ruto na wandani wake katika kundi la ‘Tangatanga’, ambao msimamo wao si kupinga wala kuunga mkono marekebisho ya Katiba. Dkt Ruto na wanasiasa wanaoegemea upande wake husema wamejitolea kuunga mkono sehemu kadhaa za kurekebisha Katiba, huku wakitaka mashauriano zaidi kabla ya kura ya maamuzi. Msimamo sawa na huu umechukuliwa na viongozi wa kidini.

Akizungumza Jumapili alipokuwa katika Kanisa la Jesus Is Alive Ministries (JIAM), Kaunti ya Nairobi, Naibu Rais alitoa wito kwa waungaji mkono wa BBI kuzuia hali ambapo patazuka ushindani wa mirengo katika suala la urekebishaji wa Katiba.

“Kuna wengi wanaoshinikiza pawepo ushindani wa ‘ndiyo’ na ‘la’. Kama ni madaraja (upatanisho) tunayotaka, basi tuachane na mambo ya mirengo. Tuna uwezo wa kushiriki mashindano lakini hatutaki kushindana kuhusu mambo ya Katiba,” akasema.

Kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa, kuna uwezekano kuwa miito ya mara kwa mara ya Dkt Ruto kwamba kura ya maamuzi ifanywe 2022, inatokana na kuwa mirengo inayotumiwa sasa katika BBI huenda ikadumu hadi wakati wa uchaguzi huo mkuu.

Gavana Kibwana, ambaye tayari ametangaza nia yake kuwania urais katika uchaguzi ujao, alisisitiza kwamba mchakato mzima wa BBI unahusu siasa za 2022.

“BBI inahusu 2022, wala si mabadiliko. Wakenya wote wanaoenzi nchi hii lazima sasa waongoze kampeni za kupinga marekebisho ya Katiba. Nitakuwa miongoni mwa wale ambao watasimama mstari wa mbele hadi mwisho kupinga. Hebu tulinde wananchi na Katiba ya 2010,” alisema Prof Kibwana hivi majuzi.

Ishara za kuwa viongozi wanatumia kampeni za BBI kujinadi kwa maandalizi ya uchaguzi wa 2022 tayari zinaonekana wazi wanapozuru maeneo mbalimbali.

Mnamo Jumamosi wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Matungu, Justus Murunga katika Kaunti ya Kakamega, viongozi wa eneo la Magharibi hawakuficha nia yao ya kulenga kufaidika uchaguzini kupitia msimamo wao wa kuunga mkono BBI.

Bw Wetang’ula aliambia jamii ya eneo hilo ifuate msimamo wake na Bw Mudavadi kwani macho yao yako kwa 2022.

“Nataka kushauri jamii ya Mulembe kwamba, tunaunga mkono BBI. Hilo tumelisema mara nyingi. Kile mnafaa muwe mnafikiria sasa ni kuhusu tu nafasi yetu baada ya BBI. Ikipita watu wa Mulembe watakuwa wapi,” akasema.

Jumapili, viongozi kutoka jamii hiyo akiwemo Bw Mudavadi na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) walikutana nyumbani kwa Seneta wa Busia Amos Wako, ikiaminika walijadiliana kuhusu mipango yao ya kisiasa.

Japo Bw Odinga husisitiza hana nia ya kutumia BBI kwa siasa za 2022, ni wazi kuwa ushirikiano wake na Rais Kenyatta umemfungulia mlango kupenya zaidi katika eneo la Mlima Kenya kuliko ilivyokuwa awali.

Vile vile, Rais Kenyatta na wanachama wa Jubilee wanaoegemea upande wake wamekuwa wakipokewa kwa shangwe wakizuru ngome za Bw Odinga, tofauti na ilivyokuwa kabla nyakati za handisheki.

Katika eneo la Rift Valley ambapo ni ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto, suala la marekebisho ya Katiba limeibua kambi mpya ya wanasiasa wanaotishia kugawanya kura za ukanda huo.

Kambi hiyo ya Seneta Moi inajumuisha pia aliyekuwa gavana wa Bomet, Bw Isaac Ruto na viongozi wengine. Katika eneo la Pwani, viongozi wanaounga mkono BBI wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho huwa hawafichi azimio lao la kuwa katika nafasi ya juu serikalini katiba ikirekebishwa ili pabuniwe nafasi ya waziri mkuu na manaibu wake.

Endapo makundi haya yatadumu hadi 2022, itakuwa vigumu kwa Dkt Ruto kudumisha ufuasi wake ambao ulikuwa tayari umeanza kupanuka hasa katika maeneo ya Kati, Magharibi na Pwani.