Misingi ya vyama vya kisiasa sharti izingatiwe katika sheria na Katiba – Muturi
Na WANDERI KAMAU
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amesema Alhamisi kuwa lazima misingi ya vyama vya kisiasa ikitwe katika Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ili kuhakikisha kuvipa nguvu kama taasisi huru.
Amesema haya kwenye hotuba katika Tamasha Kuhusu Vyama vya Kisiasa inayoendelea katika Makavazi ya Kitaifa, Nairobi.
Ni kauli ambayo pia imeungwa mkono na kinara wa Narc-Kenya Bi Martha Karua.
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ni miongoni mwa viongozi wengine waliohutubu.
Mudavadi ameonya kuwa huenda Mpango wa Maridhiano (BBI) ukasababisha migawanyiko zaidi ya kisiasa ikiwa masuala yanayozua tofauti za sasa zilizopo hayatasuluhishwa.
Tofauti hizo ni pamoja na baadhi ya watu kuzuiwa kutoa maoni yao kwa njia huru.
“Ikiwa hatutasuluhisha tofauti zilizopo kwa sasa, hali itakuwa mbaya wakati wa kura ya maamuzi,” amesema Mudavadi.