Mitishamba ilimponya binti yangu – Raila
DICKENS WASONGA na VALENTINE OBARA
KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga amefichua jinsi dawa za kienyeji zilivyomponya binti yake, Bi Rosemary Odinga ambaye alikuwa kipofu kwa miaka miwili.
Mwaka uliopita, Rosemary alifichua jinsi alivyoanza kuumwa na kichwa, akazimia wakati alipokuwa katika mkutano wa wanawake eneo la Naivasha kisha baadaye akapoteza uwezo wa kuona.
Ilibainika kuwa alikuwa na uvimbe kichwani ambao uliathiri macho yake na kumsababishia upofu.
Akizungumza Jumatano wakati wa ibada ya Krismasi katika Kanisa la Kianglikana la St Peter’s lililo Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alifichua jinsi familia yake ilivyolazimika kuzunguka kutoka hospitali moja hadi nyingine kumtafutia matibabu.
Walizuru hospitali za humu nchini na za mataifa ya nje lakini wakaambulia patupu mara nyingi.
“Tulifikia kiwango ambapo tulikuwa karibu kufa moyo kama familia kwani ziara zetu katika hospitali nyingi ikiwemo zilizo Ujerumani, Uchina na Afrika Kusini hazikuwa zinazaa matunda. Baadaye alifanikiwa kutibiwa India,” akasema.
Waziri huyo mkuu wa zamani akaongeza, “Madaktari wa Afrika Kusini walikuwa wamemwambia kuwa hataweza kuona tena maishani mwake. Lakini kuna rafiki aliyetutambulisha kwa daktari aliye India, ambaye alitumia mitishamba iliyomsaidia hadi akapona.”
Kwa mujibu wa Bw Odinga, kupona kwa Rosemary ni mojawapo ya mafanikio makubwa ambayo familia yake imepata mwaka huu na wana kila sababu ya kutoa shukrani.
Alisema binti yake alilazwa katika hospitali hiyo ya India kwa mwezi mmoja pekee.
“Wakati aliporudi kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu miezi miwili baadaye, madaktari walivutiwa sana na jinsi alivyokuwa akipona kwa kasi,” akaeleza.
Rosemary aliambia waliohudhuria ibada hiyo kuhusu maisha yake alipokuwa kipofu.
Alieleza kwamba, wakati mwingi watu walipomwona walishangaa kwa nini wanaambiwa yeye ni kipofu, kwani angeweza kuwatambua kwa urahisi na pia macho yake yalikuwa wazi.
“Nilikuwa nikisikiliza jinsi watu wanatembea kisha ninajua huyo ni mama au baba. Nikisikia sauti ya matembezi ya baba, namsalimia “hujambo baba” kisha anadhani nilikuwa nimemwona,” akasema.
Mbali na hayo, alijifunza pia kutambua sauti tofauti za watu, kwa hivyo ikawa rahisi kwake kupiga nao gumzo hata ambapo kama hawaoni.
“Macho yangu yalikuwa wazi lakini sikuwa na uwezo wa kuona. Niliporudi nchini kutoka India, niliona watoto wangu kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili. Nilifurahi sana,” akasema.
Rosemary ndiye binti mkubwa wa Bw Odinga. Alianza kuugua wakati akitarajiwa kujitosa katika siasa za eneobunge la Kibra 2017.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017, marehemu Ken Okoth ndiye aliyefanikiwa kushinda tikiti ya chama cha ODM, akaishia kushinda wadhifa huo kwa mara ya pili.
Wakati Bw Okoth alipofariki mwaka huu baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu, Rosemary alitarajiwa na wadadisi wengi kuwania wadhifa huo lakini haikuwa hivyo.
Tikiti ya ODM ilimwendea Bw Bernard Okoth ambaye ni kakaye Ken, aliyeibuka mshindi katika uchaguzi mdogo uliofanywa Novemba 7.
Wadadisi wa kisiasa hushikilia kwamba Rosemary ndiye anayeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kufuata nyayo za Bw Odinga kisiasa katika familia hiyo.