MIVUTANO zaidi inatarajiwa kati ya mirengo mbalimbali ya ODM baada ya Kiongozi wake Dkt Oburu Oginga kusema kuwa kuna mipango ya kutangaza msimamo wake kuhusu kuchaguliwa tena kwa Rais William Ruto mnamo Juni 2026.

Dkt Oginga akiongea nyumbani kwa Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, alisema kuwa chama kitafanya maamuzi kuhusu kuunga au kutounga Rais Ruto mnamo Juni mwakani.

“Tutakamilisha makubaliano yote ya kisiasa kufikia Juni 2026. Haitaenda zaidi ya Juni na ninawahakikishia hilo,” akasema Dkt Oginga, nduguye aliyekuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa chama marehemu Raila Odinga.

“Kama kiongozi wa ODM huwa sina uhuru wa kutamka lolote kama viongozi wengine. Siwezi kusema muhula mmoja au mihula miwili. Tutaketi na kurasimisha makubaliano yote kabla ya kuwapa watu wetu mwelekeo Juni 2026,” akaongeza.

Katika hotuba yake ya mwisho mnamo Septemba 2025, marehemu Bw Odinga aliwashauri wanachama wa ODM wamakinikie hoja 10 ambazo ni kigezo cha muafaka kati yao na UDA.

Dkt Oginga na baadhi ya viongozi wakuu wa ODM wameashiria hadharani kuwa wataunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili.

Kauli ya Dkt Oginga inakinzana na baadhi ya viongozi wa ODM ambao wanadai kuna mpango wa ‘kuuza chama’ kwa Rais Ruto.

“Kama ODM hatujamtuma yeyote kuzungumza kuhusu nafasi ndani ya serikali. Hatujamtuma broka yeyote kujadiliana kwa niaba ya ODM kwa serikali,” akasema Katibu wa chama Edwin Sifuna akiwa katika Kaunti ya Vihiga mnamo Jumatatu.

Gavana wa Siaya James Orengo ambaye alikuwa kwenye hafla moja na Bw Sifuna, alisema ODM itapoteza zaidi ikikubali kuingia kwenye mkataba wa kisiasa na UDA kuhusu uchaguzi mkuu wa 2027.

“ODM isiende kwenye makubaliano yoyote yasiyo rasmi kisiasa bila kufikiria na kwa vishawishi tu. Ukifanya hivyo, chama hiki kitapungua umaarufu na kuwa kidogo kuliko ilivyo kwa sasa,” akasema Bw Orengo.

Akiongea kwa Bw Wandayi, Dkt Oginga aliashiria kuwa watamuunga mkono Rais Ruto kwa sababu hiari ni kuchagua kati ya kiongozi wa nchi na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Wandayi naye aliwashutumu viongozi wanaopinga Serikali Jumuishi akisema siasa tupu haileti umoja au hadhi jinsi marehemu Bw Odinga alivyosema.

“Wale ambao wanapiga kelele hapo nje hawakuwa tukijadiliana kuhusu Serikali Jumuishi. Raila alikuwepo,” akasema Bw Wandayi.

“Hii ni serikali ambayo hatukuichagua lakini kupitia Raila tukapewa nafasi sita za juu,” akaongeza.

Waziri huyo alisisitiza kuwa ODM itaingia kwenye mkataba na Kenya Kwanza kwa sababu lengo lao ni kuwa serikalini 2027.

“Katika muungano unaacha hiki na kupewa kile mradi kuwe na maelewano. Wale wanaopiga kelele wanafanya hivyo mapema sana,” akaongeza.