HabariSiasa

Mlima Kenya kubuni chama cha kisiasa kabla ya 2022

November 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na ALEX NJERU

VIONGOZI wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya Mashariki wameanzisha harakati za kubuni chama kimoja cha kisiasa ielekeapo 2022.

Akiwahutubia wanahabari katika eneobunge la Maara Jumatano, aliyekuwa gavana wa Tharaka-Nithi Samuel Ragwa (pichani) alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa eneo hilo lina chama kimoja cha kisiasa ambacho kitawaleta pamoja wakazi wa sehemu hiyo kabla ya uchaguzi huo.

“Tumekutana mara kadhaa kama wanasiasa katika eneo hilo na kuamua kwa pamoja kubuni chama ambacho kitatuunganisha ielekeapo 2022,” akasema Bw Ragwa.

Alieleza kuwa, ili kuepuka mivutano ya chama na viongozi walio mamlakani, wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi uliopita tayari wameanza mchakato wa kubuni chama hicho. Kulingana naye, taratibu hizo zinaendeshwa kwa ushirikiano na asasi husika.

Alieleza kuwa msukumo mwingine pia unatokana na nia ya kutaka kuimarisha usemi wao wa kisiasa, hasa kuhusu mchakato wa uteuzi wa naibu mgombea urais.

Aliomba uwepo wa umoja wa kisiasa kati ya kaunti za Meru, Embu, Tharaka-Nithi na hata Isiolo, akisema hilo litaongeza usemi wao wa kisiasa kuhusu atakayekuwa naibu mgombea urais au hata atakayekuwa mgombea urais.

Alisema kuwa viongozi wote wakuu wa chama hicho watatoka katika kaunti zote, ili kuhakikisha hakuna mivutano yoyote ya uongozi inayotokea.

Alieleza kwamba ingawa viongozi wengi katika kaunti hiyo wamechaguliwa kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP) watamuunga mkono Naibu Rais William Ruto kwa sharti kwamba lazima amteue naibu mgombea wake kutoka eneo hilo.

Alionya kwamba huenda wakamuunga mkono mgombea mwingine ikiwa wito wao hautazingatiwa.

“Chama hicho kitakuwa jukwaa letu kama vile chama cha Amani National Congress (ANC) cha Magharibi, Wiper cha Ukambabi au ODM cha eneo la Luo Nyanza,” akasema.

Bw Ragwa alisema kaunti ya Tharaka Nithi imefaidika kwa kiwango kidogo licha ya kuiunga mkono serikali ya Jubilee kwenye uchaguzi wa 2017.

Alieleza kuwa chama kitawateua wawaniaji katika nyadhifa mbalimbali, ikiwezekana hata baada ya uchaguzi wa 2022. Eneo hilo limekuwa likilalamikia kutengwa katika mikakati ya kisiasa katika sehemu zingine za Milma Kenya.