Mlima Kenya ndio wanaogopa Covid-19 zaidi – utafiti
Na CHARLES WASONGA
WAKAZI wa eneo la Mlima Kenya wanaogopa zaidi ugonjwa wa Covid-19 kuliko wakazi wa maeneo mengine nchini, ripoti ya utafiti imefichua.
Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi na Shirika la Utafiti la TIFA, asilimia 72 ya wakazi hao waliohojiwa walikiri kuogopa ugonjwa huo zaidi.
Ni asilimia tisa pekee kati yao ambao ilibainika kuwa hawana wasiwasi kuhusu janga hilo la kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo.
Maeneo yenye yenye wakazi wengi wanaoogopa maambukizi ya Covid-19 ni; Mashariki (asilimia 69), Nyanza (67), Pwani (64) huku asilimia 52 ya wakazi wa Nairobi wakiwa na wasiwasi wa kuambukizwa ugonjwa huo.
Kwa ujumla, utafiti huo ambao uliendeshwa kati ya Juni 7 na Juni 21, 2020, umebainisha kuwa asilimia 65 ya Wakenya wanahofia kuambukizwa Covid-19. Na asilimia 16 ya Wakenya hawana wasiwasi wowote.
Jumla ya watu 843 waliohojiwa katika utafiti huo ambao uliendeshwa katika maeneo yote nane nchini ambayo zamani ilijulikana kama mikoa.
Utafiti huo pia uligundua kuwa asilimia 79 ya waliohojiwa wako tayari kujiwasilisha kwa upimaji kubaini ikiwa wana virusi vya corona.
Na asilimia 10 walisema hawako tayari kujiwasilisha kwa upimaji.
Kati ya wale ambao wako tayari kupimwa hata hivyo wanahofia kuwa shughuli hiyo ni uchungu na kando na kuogopa kupelekwa katika vituo vya kujitenga kwa lakini pamoja na kutengwa na majirani.
Miongoni mwao wale watu ambao hawako tayari kujitoza kupimwa corona, asilimia 39 wanasema shughuli hiyo inasababisha usumbufu, asilimia 10 wanasema wanahofia kuwekwa karantini huku asilimia nane wakisema hawataki kupimwa kwa hofu ya kutengwa na majirani zao endapo watapatikana na virusi hivyo.