Habari

Mmiliki nyumba ang'oa paa, avunja milango akidai kodi

April 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

FAMILIA nne katika mtaa wa Mikindani eneobunge la Changamwe, zimeachwa bila makao baada ya mwenye nyumba kuwang’olea milango na mabati kwa kukosa kulipa kodi.

Mmoja wa waathiriwa hao, Bi Ruth Omumia, 38, na mumewe Bw Joseph Omumia, wamesema kilio chao kwa mwenye nyumba hiyo kutowang’olea mabati hakikufua dafu.

Bw Omumia ni mmoja wa zaidi ya vibarua 100 walioachishwa kazi kutoka kwa kiwanda cha utengenezaji na kusafirisha bidhaa (Export Processing Zone) kilichoko Changamwe kufuatia athari za janga la corona.

Wawili hao waliokodi chumba kimoja, wanatakiwa kulipa kodi ya Sh3,000 kila mwezi.

“Aprili 20, 2020, mwenye nyumba alikuja kudai kodi ambapo tulimsihi kutupa muda zaidi wa kulipa lakini alikataa. Tuliambiwa tulipe ama tutoke kwa nyumba yake. Tarahe 27 akatuma watu kuja kung’oa milango na mabati,” amesema Bi Omumia.

Mwanamke huyo alisema wanadaiwa kodi ya miezi mitatu.

Bi Omumia na mumewe sasa wamelazimika kuwapeleka watoto wao wawili kuishi na mwalimu wao.

Aidha Bi Omumia amesema japo walimuomba mwenye nyumba achukue pikipiki ya mumewe hadi pale watakapopata uwezo wa kulipa deni lao, alikataa.

“Hatuna pahala pa kwenda na tunaomba wahisani kutusaidia kwani tangu kutolewa mabati tumekuwa tukinyeshewa,” akasema.

Wawili hao wamesema waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Mikindani.

Sehemu ya nyumba ambamo Bi Ruth Nyakowa Omumia na mumewe huishi lakini paa liling’olewa walipochelewa kulipa kodi. Anaonekana katika picha hii ya Aprili 30, 2020. Picha/ Laban Walloga