Moi alikataa niwe Rais
MARY WANGARI na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais, Dkt William Ruto, hatimaye amefichua kuwa uhusiano wake na aliyekuwa mlezi wake wa kisiasa, Daniel arap Moi, ulivurugika alipotangaza nia yake ya kugombea urais.
Dkt Ruto alisema kwamba tangu wakati huo, uhusiano wake na Mzee Moi ulianza kuwa baridi tofauti na kabla ya kutangaza azma yake.
“Tulikuwa na mkutano mjini Eldama Ravine ambapo nilitangaza azma yangu ya kuwania urais. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mafarakano yetu,” alieleza Bw Ruto.
Alisema kuanzia wakati huo Mzee Moi aliacha kumchangamkia kama awali na hata kumdhalilisha hadharani.
Kulingana na Naibu Rais, hakuchukulia tukio hilo kwa uzito hadi alipofungiwa nje ya lango la boma la Mzee Moi pamoja na wabunge wengine 15 walipoenda kumtembelea rais huyo mstaafu.
Dkt Ruto alisema walinzi waliwaarifu kwamba Mzee Moi hakutaka kukutana na mtu yeyote wakati huo.
Kabla ya tukio hilo, uhusiano wa Ruto na Moi ulikuwa mzuri. Alikuwa mmoja wa wanasiasa chipukizi kutoka jamii ya Wakalenjin ambao Mzee Moi alikuza.
“Kutoka Eldama Ravine nilifikiri ni kitu rahisi. Tulikuwa wabunge 15 na ilikuwa kawaida yetu kila mara tulipokuwa Nakuru, kumtembelea Mzee na kushiriki kikombe cha chai, kuzungumza kidogo kabla ya kurejea makwetu,” alisema akizungumza na runinga ya Citizen mnamo Alhamisi usiku.
“Safari hii tulipata lango likiwa limefungwa na tukaarifiwa kwamba Mzee hakutaka kukutana nasi,” alisimulia.
Aidha, Bw Ruto alieleza jinsi marehemu alivyotoa matamshi aliyohisi yalimdunisha alipopuuzilia mbali nia yake ya kugombea urais na zaidi uwezo wake wa kuongoza jamii.
Rais Moi, kulingana na Bw Ruto, alikuwa ameteua watu mbalimbali alioamini walikuwa na uzoefu wa siasa si tu katika jamii ya Bonde la Ufa bali pia katika ulingo wa siasa nchini.
Alisema hapo ndipo alipogundua kwamba mtu aliyemtazama kama kielelezo chake kisiasa alikuwa na mawazo tofauti na yake.
“Alitamka maneno ya kudhalilisha mno tangazo langu, akipuuza azma yangu na kusema nilikuwa ninapotosha jamii. Bw Moi alijitokeza na kusema Ruto hawezi kuwa kiongozi, mnapaswa kuchagua watu wenye ujuzi kama Bw Henry Kosgei na Bw Nicholas Biwott. Ninakumbuka wakati huo nikifafanua kwamba sikutaka kuwa kiongozi wa jamii bali niliazimia kuwa Rais,” alisema Dkt Ruto.
Matamshi ya Bw Ruto yamejiri huku Wakenya wakitazamiwa kutoa heshima za mwisho kwa Mzee Moi aliyefariki Jumanne, Februari 2, 2020, ambapo ripoti ziliibuka kwamba Naibu Rais alikuwa amezuiwa kuona mwili wa marehemu katika mochari ya Lee Funeral Home jijini Nairobi.
Mnamo Mei 2018 Dkt Ruto alimtembelea kiongozi huyo nyumbani kwake Kabarak lakini hakuweza kukutana naye huku ripoti zikiashiria kwamba Mzee Moi alikataa kukutana na Naibu Rais kutokana na chuki kati yao.
Hata hivyo, msemaji wa Bw Moi, Lee Njiru alieleza kwamba Rais huyo wa zamani alikuwa akifanyiwa uchunguzi na madaktari wake ndiposa mkutano huo haukufanyika.
Dkt Ruto na mwanawe Moi, Gideon ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Baringo na mwenyekiti wa chama cha Kanu wamekuwa wakipigania ubabe wa kisiasa kila mmoja akitaka kuwa msemaji wa jamii ya Wakalenjin.
Wadadisi wanasema Gideon anapambana kudumisha jina la familia ya Moi katika ulingo wa kisiasa nchini.