Habari

Morara ajeruhiwa na kutimuliwa alipojaribu kutoa maoni kuhusu Gachagua huko Bomas

Na DANIEL OGETTA, BENSON MATHEKA October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKILI na mwanaharakati  Morara Kebaso alilazimika kutoroka baada ya kuzomewa alipofika ukumbi wa Bomas of Kenya wakati wa ushirikishaji wa umma kuhusu kuondolewa ofisini kwa Naibu Rais Gachagua.

Mkosoaji huyo wa serikali ya Kenya Kwanza mwenye umri wa miaka 28 alijeruhiwa ghasia zilipozuka alipokuwa akijaribu kupanda jukwaani.

Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha akirushiwa  viti na hali ya wasiwasi ilipozidi, hakuwa na la kufanya ila kutoroka.

“Nilizuiwa kuingia Bomas langoni. Nilipoingia, nilinyimwa maikrofoni. Ghasia zilizuka. Nimeumia. Naelekea hospitali. Nitazungumza siku nyingine,” alichapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X, muda mfupi baada ya tukio hilo.

Mwanaharakati huyo  amekuwa akifanya ziara kote nchini kukagua miradi ya serikali iliyokwama ili kufichua ulegevu wa wale walio  mamlakani.

Amekuwa akitumia umaarufu aliopata katika mitandao ya kijamii kufichua jinsi mabilioni ya pesa zimetumiwa vibaya katika miradi feki kote nchini.

Tukio la Ijumaa lilijiri siku chache baada ya kukamatwa na polisi na kushtakiwa kwa makosa yanayohusiana na  matumizi ya mtandao na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000.