Habari

Msaidizi wa Rais Moi, akosoa kauli ya Museveni

Na FRANCIS MUREITHI November 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA msaidizi wa Rais Mstaafu Hayati Daniel Moi, Lee Njiru amemuonya Rais wa Uganda Yoweri Museveni dhidi ya kutoa kauli za uchochezi ambazo zinaweza kuzorotesha uhusiano wake na nchi jirani

Kulingana na Bw Njiru, matamshi kama hayo ni kama ‘kuuma mikono iliyowahi kumlisha.’

Bw Njiru, ambaye kwa miongo kadhaa aliishi Ikulu wakati wa utawala wa Rais Daniel Moi, alifichua jinsi Rais Museveni akiwa kiongozi wa waasi alitumia afisi yake jijini Nairobi kama kituo cha kutoa amri wakati wa vita vya kijamii Uganda miaka ya 1980.

Hapo ndipo Rais Museveni aliendeleza maasi na hatimaye kumwondoa madarakani Rais Milton Obote mnamo 1986.

Bw Njiru pia alikumbuka jinsi ndege za Jeshi la Wanahewa wa Kenya zilivyotumiwa na Rais Museveni kuingia Uganda kupitia Rwanda alipokuwa akitaka kunyakua mamlaka.

“Tulizoea kumpa maafisa wetu wa usalama wa kijeshi, ambao walimsindikiza kwa ndege za Kenya Air Force Buffalo ili aweze kufika Luwero Triangle (sehemu ya Uganda ambako waasi walikuwa wakiishi) wakati wa vita vya msituni,” alisema Bw Njiru.

“Je, (Rais Museveni) anawezaje kuwatishia watu waliomweka madarakani?”

Aliongeza kuwa kiongozi huyo wa Uganda ana mengi ya kuishukuru Kenya badala ya kutoa vitisho.

Bw Njiru alikuwa akijibu tamko la hivi majuzi la Rais Museveni.

Matamshi hayo yalizua hasira nchini Kenya, huku wengi wakiyafasiri kuwa ni tishio kwa amani ya eneo hilo.

“Iwapo Rais Museveni anataka kuingia bila vikwazo katika Bahari ya Hindi, anapaswa kuketi na Rais William Ruto wa Kenya na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na kuunda sheria inayokubalika na wote,” akasema Bw Njiru.

“Katika makubaliano kama hayo, nchi hizo tatu zitamiliki kwa pamoja ufuo wa Bahari ya Hindi, mafuta ya Uganda katika Bonde la Ziwa Albert, gesi ya Tanzania Mtwara na Lindi, na dhahabu ya Kenya huko Ikolomani,” alisema Bw Njiru.