Mshtuko GSU akiua mke, mtoto na kujimaliza kwa risasi
WAKAZI wa mjini Mokowe, Kaunti ya Lamu, wamebaki kwa mshtuko baada ya afisa wa kitengo cha polisi cha GSU kuwaua kwa risasi mkewe na mtoto mwenye umri wa miaka mitano, kabla kujipiga risasi na kufariki.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Lamu Kipsang Changach, alithibitisha mauaji hayo yaliyotokea mwendo wa saa kumi na mbili unusu asubuhi Jumapili.
Bw Changach alisema afisa aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa anahudumu katika kambi ya GSU iliyo viungani mwa mji wa Mokowe.
Kulingana na Bw Changach, mauaji yalitokea kwenye nyumba ambayo afisa huyo alikuwa amekodisha wakiishi na mwanamke huyo katikati mwa mji wa Mokowe.
“Tumeamkia tukio ambapo afisa wa GSU kutoka kambi ya Mokowe amepatikana kwenye nyumba moja mjini hapa akiwa amewaua mke na mtoto na kisha kujitoa uhai kwa bunduki.
“Tunashuku mauaji yanatokana na mzozo wa kinyumbani. Tumeanzisha uchunguzi. Miili tayari imesafirishwa hadi hifadhi ya maiti katika Hospitali ya Malindi, Kaunti ya Kilifi kwa upasuaji,” akasema Bw Changach.
Kamanda huyo hata hivyo aliwashauri maafisa wa polisi wanaokumbwa na msongo wa mawazo na matatizo mengine kujitokeza kupokezwa ushauri nasaha badala ya kukimbilia kujiua na kuathiri wengine.

“Afisa hakuonyesha dalili yoyote kwamba alikuwa akipitia matatizo. Alitoka kambini kama kawaida kwenda nyumba aliyokodi na mkewe na mtoto ambayo iko nje ya kambi.
“Tunashangaa kuarifiwa kwamba ametekeleza mauaji hayo. Maafisa wangu wawe na tabia ya kutafuta ushauri kwa wenzao na hata wakubwa wao wanapopitia changamoto. Kujiua na kuua wengine siyo suluhu,” akasema Bw Changach.
Mmoja wa majirani wa wanandoa hao, Bw Mohamed Yusuf, alieleza kushangazwa na tukio hilo.
“Tunawafahamu wawili hawa kama wapenzi. Wameishi nasi kwa karibu mwaka mmoja sasa. Mama ni mwalimu ilhali mume ni polisi wa GSU. Hatujawahi kusikia wakizozana. Mauaji yametupata kwa mshangao mkuu,” akasesma Bw Yusuf.
Mtaalamu wa Masuala ya Kisaikolojia na Ushauri Nasaha anayehudumia Hospitali ya Mpeketoni, Bw Andrew Masama, aliwasihi wanandoa na wapenzi kuwa wazi ili kuepuka migogoro nyumbani.
Alisema maafisa wa polisi mara nyingi tayari hupitia changamoto tele na msongo wa mawazo karibu kila siku kazini.
“Ombi langu kwa wanandoa na hata wapenzi ni kwamba tuweni na uwazi ili kuepuka migogoro na mauaji. Pia tutafute ushauri nasaha tunapokumbwa na changamoto za maisha, ziwe za kikazi au kijamii,” akasema Bw Masama.