Msiogope kutukosoa, Rais aambia viongozi wa kidini nchini
JUMA NAMLOLA na PSCU
RAIS Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa kidini wajitokeze waziwazi na kukemea maovu katika jamii.
“Ongeeni wazi na kwa ujasiri dhidi ya maovu yanayoirudisha nyuma nchi yetu. Kazi yetu ya kujenga taifa ni jukumu la pamoja kwani tunahudumia wananchi hao hao. Kwa upande wetu, tutawatimizia wananchi mahitaji yao ya masuala ya kidunia, nyinyi mkiwatimizia ya kiroho,” akasema.
Alikuwa akiwahutubia viongozi wa kidini waliomtembelea katika Ikulu ya Nairobi, ambapo alisema nchi inakumbwa na changamoto nyingi zinazoweza kutatuliwa kupitia ushirikiano wa Wakenya wote, wakiwemo viongozi hao wa kidini.
“Napongeza juhudi za viongozi wa Kanisa katika kukemea ufisadi. Lakini hiyo haitoshi. Kuna fursa ya kufanya mengi zaidi. Hili ni jukumu letu sote, si la kuachiwa serikali pekee,” akasema.
Kauli ya rais Kenyatta kwa viongozi inaonyesha jinsi ambavyo wamenyamaza, wakilinganishwa na watangulizi wao.
Maaskofu Alexander Muge, Manasses Kuria, David Gitari, Ndigi Mwana a Nzeki na Makasisi Timothy Njoya na Mutava Musyimi walikuwa katika mstari wa mbele kukosoa serikali na jamii kwa jumla katika masuala mengi.
Jana, Rais Kenyatta aliwafafanulia viongozi wa kidini kwamba kukosoa maovu si siasa, na kamwe hawana sababu ya kuogopa kukemea ufisadi, uhalifu, utovu wa usalama kati ya maovu mengine nchini.
Rais Kenyatta na viongozi hao walikubaliana kuandaa maombi ya kitaifa Jumamosi, Oktoba 10, ili kuiombea nchi inapokumbwa na matatizo mengi, likiwemo janga la Covid-19.
Aliwatwika viongozi hao jukumu la kuwaongoza Wakenya ‘kuunda madaraja’ ya kujichukulia kuwa kaka na dada katika familia na jamii kwa jumla.