Mswada kielelezo watua bungeni wabakaji wakatwe uume
Na CHARLES WASONGA
MUUNGANO wa wabunge wa kike kutoka jamii za wafugaji sasa unapendekeza kuwa sheria kuhusu dhuluma za kimapenzi ifanyiwe marekebisho ili wabakaji waadhibiwe kwa kukatwa uume.
Katibu Mkuu wa muungano huo Bi Rehema Jaldesa Alhamisi alisema kuwa amewasilisha mswada kielelezo kwa afisi ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi akipendekeza mabadiliko kwa kipengee cha 43 cha sheria hiyo.
“Nimewasilisha pendekezo langu kwa Spika wa Bunge kwa njia ya mswada wa marekebisho nikitaka adhabu ya kifungo cha miaka 10 kwa wale watakaopatikana na hatia ya kuwabaka wasichana wadogo ibadilishwe na badala yake nyeti zao zikatwe,” akasema.
Bw Jaldesa ambaye ni Mwakilishi Mwanamke wa Isiolo alisema adhabu hiyo ndio njia mwafaka ya kumaliza unyama huo ambao hutendewa watoto wa kike hasa katika jamii za wafugaji.
“Haina haja kwa mwanamume ambaye amembaka mtoto wa kike kufungwa jela kwa miaka 10 baada ya kuharibu kabisa maisha ya mhasiriwa huyo?” akauliza.
Bi Jaldesa alitoa mfano wa hali ilivyo nchini Arabia ambapo wizi umemalizwa kabisa kutokana na adhabu ya wezi kuwakata mikono wanapopatikana na hatia.
“Hata hivyo, nia yangu sio kuona wanaume wasio na hatia wakikandamizwa bali wale ambao wana tabia mbaya ya kuwabaka hata watoto wao wenyewe,” akasema.
Mbunge huyo alisema hayo jana katika mkahawa wa Intercontinental, Nairobi wakati wa uzinduzi rasmi ya muungano huo ambao ni kitengo cha Kundi la Wabunge kutoka Jamii za Wafugaji (PPG).
Miongoni mwa waliohudhuria shughuli hiyo ni wabunge Soipan Tuya (mbunge mwakilishi, Narok), Sarah Korere (Laikipia Kaskazini), Ruweidha Obbo (Mbunge Mwakilishi, Lamu), Janet Teyia (Kajiado), Abushiro Halake (Seneta Maalum) na Naomi Jillo (Seneta Maalum)
Bi Jillo ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo alisema lengo lao ni kupambana na maovu ambayo yamedunisha mtoto wa kike na wanawake katika jamii zao.
“Nia yetu ni kupambana na maovu kama vile ubakaji wa wanawake na watoto wa kike, ukeketaji wa wasichana, ndoa za mapema na kutengwa kwa mwanamke katika masuala ya umiliki wa ardhi na uwakilishi wa kisiasa,” akasema.
Bi Jillo alisema njia mwafaka ya kukomesha maovu hayo ni kuendeleza uhamasisho ili wanawake wengi waweze kupigania nafasi za uongozi kupitia chaguzi.
“Ni fahari yetu kwamba kufikia sasa idadi ya wabunge na maseneta wa kike ni 28 ambayo walichaguliwa au kuteuliwa katika uchaguzi mkuu. Kwa mfano, kwa mara ya kwanza mwanamke amechaguliwa kuwa seneta katika eneo la Kaskazini mwa Kenya… na huyo sio mwingine ila Bi Fatuma Dullo,” akasema.
“Katika uchaguzi wa 2022 tunamatumaini kwa wanawake wengi watachaguliwa kuwa magavana, meseneta na wabunge,” Bi Jillo akaongeza.