Habari

Mtihani wa KCSE 2019 wafika tamati

November 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MTIHANI wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) umekamilika Jumatano huku Wizara ya Elimu ikisema visa vya majaribio ya baadhi kufanya udanganyifu viliripotiwa katika vituo 21 kati ya zaidi ya vituo 10,000 kote nchini.

Akiongea katika shule ya upili ya Jamhuri, Nairobi siku ya mwisho ya mtihani huo, Waziri wa Elimu George Magoha alifichua kuwa jumla ya simu 90 zilipatikana katika vituo mbalimbali lakini akafafanua kuwa hazikutimiwa kuiba mtihani huo.

“Simu hizi zilipatikana kabla ya kutumika katika wizi wa mtihani. Kwa hivyo, ningependa kuwahakikisha Wakenya kuwa wizi wa mtihani haukufaulu hata katika vituo 21 ambako simu hizo zilipatikana,” akasema Profesa Magoha.

Alisema maafisa wa wizara yake na wale wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchi (KNEC) walikuwa macho zaidi katika shule 300 baada ya kupata habari za kijasusi kuhusu uwezekano wa kutokea udanganyifu.

Alisema baadhi ya shule hizo zinapatikana katika eneo la Eastleigh, Nairobi, Kisii, Homa Bay, Migori, Wajir na Garissa.

Hata hivyo, waziri alisema watu 45 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali ya kujaribu kuiba, au kufanikisha wizi wa mtihani huo na wamewasilisha mahakamani.

Profesa Magoha ambaye alikuwa ameandamana na Katibu wa Wizara hiyo anayesimamia Elimu ya Msingi Belio Kipsang, kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Knec Mercy Karogo na mwenzake wa Tume ya Huduma kwa Walimu Nancy Macharia, amekariri kuwa matokeo ya mtihani yatatangazwa kabla ya sikukuu ya Krismasi.

Waziri amesema shughuli ya usahihishaji itaanza wiki ijayo na itadumu kwa muda wa majuma matatu pekee. Na jumla ya walimu 33,000 watashiriki katika shughuli hiyo.

“Mipango yote ya kuanza kwa usahihishaji imekamilika na shughuli hiyo itaanza Jumatatu. Watahiniwa watajua matokeo yao kabla ya Desemba 25, 2019,” akasema Waziri Magoha.

Jumla ya watahiniwa 669,745 walifanya mtihani wa KCSE mwaka 2019 na ambao ulianza mnamo Novemba 4.

Mwaka 2018 matokeo ya wanafunzi 100 yalifutuliwa mbali baada ya kubainika kuwa walishiriki udanganyifu. Na jumla ya walimu 14 walipigwa kalamu kwa TSC baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kuiba mtihani huo.