Muda maalum wa sensa wakaribia kutamatika baadhi wakihofia kukosa kuhesabiwa
Na SAMMY WAWERU
ZIMESALIA siku mbili pekee kukamilika kwa muda uliotengwa maalumu kwa shughuli ya kitaifa ya kuhesabu watu, sensa 2019.
Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wameelezea hofu yao kwamba huenda wakakosa kuhesabiwa.
Kulingana na msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna, shughuli hiyo iliyoanza Jumamosi Agosti 24 itatamatika Jumamosi Agosti 31.
Kwenye kikao na waandishi wa habari Jumatano, Kanali Oguna alisema wale ambao hawatakuwa wamehesabiwa baada ya Agosti 31 watatakiwa kuripoti katika afisi ya chifu au kamishna wa kaunti.
Kufikia Jumatano, baadhi ya wananchi walilalamikia kutoona makarani wa taasisi ya takwimu za kitaifa (KNBS) katika maboma yao, wakihofia kufungiwa nje katika shughuli hiyo.
Awali Bw Oguna alikuwa amesema watu wasiwe na wasiwasi, akihakikisha kwamba kila Mkenya atashirikishwa.
Edwin Kabeti ambaye ni mkazi wa Nairobi anasema kufikia sasa maafisa wa KNBS hawajaonekana katika jengo analoishi.
“Nimekuwa nikiwasubiri kuanzia Jumamosi na sioni dalili yao kunihesabu,” Bw Kabeti ameambia Taifa Leo.
Shughuli hiyo ya kitaifa iliendeshwa mnamo Jumamosi na Jumapili kati ya saa kumi na mbili za jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi.
Jumapili, Kanali Oguna alisema baada ya Agosti 24 na 25, shughuli hiyo itafanyika hata wakati wa mchana.
Bi Annitah Wairimu kutoka Kiambu anapendekeza ili kuhesabu kila Mkenya maafisa wa KNBS waruhusiwe kuzuru maeneo ya kazi kujua wale ambao hawajashirikishwa.
“Nina wasiwasi huenda muda uliotengwa ukaisha kabla sijahesabiwa. Ninaomba serikali iamuru KNBS maafisa wake wazuru watu katika maeneo yao ya kazi, wale ambao pamoja na jamaa zao hawajahesabiwa data zao zichukuliwe. Baadhi yetu tunafanya ajira za juakali zinazotulazimu kuamkia alfajiri na mapema na kutoka kama tumechelewa,” anasema Annitah.
Kauli ya mfanyabiashara huyo pia inaungwa na Bw Simon Kagombe anayelalamikia kukawia kwa maafisa hao.
Naye Bi Mary Wanjiru ambaye ni mmoja wa makarani wanaoendesha shughuli hiyo eneo la Zimmerman, amesema kwamba katika mengi ya majengo wanayozuru mchana, wanakaribishwa na kufuli mlangoni.