Habari

Mudavadi akataa robo mkate

July 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON AMADALA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, amejitenga na mipangilio ya kisiasa inayoendelea nchini, ambapo huenda baadhi ya wanasiasa wa ‘upinzani’ wakateuliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika baraza la mawaziri.

Bw Mudavadi alisema mpango wa kubuni nafasi zaidi serikalini miaka miwili tu kabla ya uchaguzi ni mchezo wa siasa.

Kumekuwepo na ripoti kuwa Rais Uhuru Kenyatta ana mpango wa kuwashirikisha vigogo wa siasa za kimaeneo serikalini kwa kuwapa fursa ya kupendekeza watu wao kuteuliwa katika baraza la mawaziri.

Vigogo hao ni pamoja na Raila Odinga (ODM), Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Gideon Moi (Kanu).

Bw Mudavadi alisema Ijumaa kuwa hana haja na cheo serikalini, akitaja mpango wa Rais Kenyatta kama njama ya kutatiza mipango yake ya kuwania urais 2022.

Alieleza kuwa alipata funzo kubwa mnamo 2002 wakati alipoteuliwa kuwa makamu wa rais kwa miezi mitatu pekee na marehemu Rais Daniel Moi, jambo lililomfanya hata kushindwa kuhifadhi kiti chake cha ubunge katika eneo la Sabatia.

“Sitaki kurudia makosa niliyofanya na kuathiri safari yangu kisiasa. Lengo langu ni kuwatumikia Wakenya kama rais baada ya uchaguzi ujao. Sitaki kufumbwa macho na mambo yanayoendelea serikalini kwa sasa,” akasema.

Alisisitiza kuwa suala kuu ambalo Rais Kenyatta anapasa kuwa akishughulikia wakati huu ni kufufua uchumi ambao umezorota.

“Uchumi wetu umeharibika na unahitaji kufufuliwa. Serikali inapaswa kushughulikia masuala ya deni la taifa kwa kuona vile ulipaji wake unaweza kulainishwa,” akasema.

KUKOSOA SERIKALI

Kwenye mahojiano katika vituo vya redio vya Mulembe, Sulwe na Vuka mnamo Ijumaa, kiongozi huyo alisisitiza kuwa ataendelea kutekeleza majukumu yake ya kuikosoa serikali hadi uchaguzi utakapofika.

Aliwaomba Wakenya kutathmini kwa kina utendakazi wa viongozi wanaopania kuwania urais hapo 2022, kwa kumchagua kiongozi atakayeimarisha uchumi wa nchi na kukabili ufisadi.

“Lengo langu si kuwa kiongozi wa eneo la Magharibi. Nataka kuwaomba Wakenya wote kunipa nafasi kuwahudumia kama rais wao hapo 2022,” akasema.

Kuhusu mikakati ya serikali kufufua sekta ya sukari, kiongozi huyo alisema kuwa hatua ambazo zilitangazwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya hazijajumuishwa kwenye bajeti.

Mpango huo ni tangazo la serikali kuviondolea viwanda vya sukari deni la Sh58 bilioni.

Alisema kuwa ahadi zinazotolewa na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Gavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo la magharibi ni njama ya kuwahadaa wenyeji.

“Ukiangalia kwa kina bajeti iliyosomwa majuzi, hakuna lolote lililoelezewa kuhusu fedha zilizotengewa miradi hiyo. Hilo linamaanisha kuwa mkutano ambao Wamalwa, Oparanya na Atwoli walifanya na Rais hautawafaidi wakazi,” akasema.

Pia alipuuzilia mbali wale wanaomkosoa yeye pamoja na Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma) kwa kutounga mkono miito ya umoja wa kisiasa wa jamii ya Abaluhya ili kumchagua kiongozi mmoja kutoka eneo hilo kuwania urais.