Mudavadi hahitaji ‘baraka’ za Raila 2022, ANC yasema
Na DERICK LUVEGA
UHASAMA kati ya vyama tanzu wa Nasa – ODM na ANC – unaendelea kutokota baada ya ANC kuambia ODM kwamba kiongozi wake, Musalia Mudavadi hahitaji ‘baraka’ za Raila Odinga katika azma yake ya kugombea urais 2022.
Msemaji wa Bw Mudavadi Kibisu Kabatesi, katika taarifa aliambia chama hicho cha chungwa kwamba Mudavadi hatamani kutawazwa na Bw Odinga au mtu yeyote kuwa mgombeaji urais wa upinzani katika uchaguzi mkuu ujao.
Bw Kabatesi alitoa kauli hiyo akielezea kukerwa na matamshi yaliyotolewa na viongozi wa ODM wakiendesha kampeni katika eneo bunge la Kibra ambapo ilidaiwa walitumia lugha ya matusi dhidi ya Bw Mudavadi.
Aliyataja matamshi hayo kama ‘takataka’.
Inasemekana kuwa viongozi wa ODM wamekerwa na uamuzi wa ANC wa kufadhili mgombeaji katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Kibra ambao utafanyika Novemba 7.
Mpeperushaji bendera wa ANC katika kinyang’anyiro hicho ni aliyekuwa meneja wa kampeni za urais za Bw Odinga kwenye uchaguzi wa 2013, Bw Eliud Owalo.
Mwanasiasa huyo aligura ODM Agosti 2019 na kujiunga na ANC ambapo alipewa tiketi ya moja kwa moja kuwania kiti hicho kilichosalia wazi kufuatia kicho cha Ken Okoth.
Ford Kenya
Chama cha Ford Kenya nacho kimemdhamini Khamisi Butichi kuwania nafasi hiyo huku bendera ya ODM ikipeperushwa na kaka yake marehemu Okoth Benard Imran Okoth.
Uamuzi wa vyama hivyo kudhamini wagombeaji katika uchaguzi huo umekera chama hicho kinachoongozwa na Bw Odinga kikiufasiri kama usaliti.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alisema vyama hivyo vimehujumu moyo wa umoja ndani ya Nasa kwa kuwasilisha wagombeaji katika kinyang’anyiro hicho.
“Kibra ni ngome yetu kama ODM na ni usaliti mkubwa kwa wenzetu kudhamini wagombeaji. Mgombeaji wetu alitosha kuwakilisha muungano wa NASA katika uchaguzi huo,” akasema.
Kulingana na Bw Sifuna, Bw Mudavadi hakushauriana na Bw Odinga kuhusu uamuzi wa chama chake kudhamini mgombeaji.
“Ningependa kumwambia Musalia na chama chake cha ANC kwamba wamezima uwezekano wowote wa vyama tanzu vya Nasa kufanya kazi pamoja katika katika chaguzi zijazo,” Bw Sifuna akasema.