MUGO WA WAIRIMU: Daktari kutoka kuzimu
Na WAANDISHI WETU
‘DAKTARI’ bandia Mugo wa Wairimu, ambaye alishtakiwa miaka mitatu iliyopita kwa kuhusika katika visa vya uhalifu ikiwemo madai ya kubaka wagonjwa wakiwa hali mahututi baada ya kuwanywesha dawa za kulewesha, anatafutwa tena na maafisa wa polisi.
Hii ni kufuatia ufichuzi wa kina wa televisheni ya NTV, ambao uligundua kuwa badala ya kuacha vitendo vilivyomfanya kukamatwa na kushtakiwwa mnamo 2015, mwanamume huyo ambaye jina lake halisi ni James Mugo Ndichu, alihamisha kliniki yake kutoka mtaa wa Githurai 44 hadi Kayole jijini Nairobi.
“Tunamkana kabisa mkora huyo; kamwe yeye si mwuguzi. Vitendo anavyovifanya ni vya kishetani. Ushahidi upo wa wazi. Hakuna lingine linalohitajika kumfunga jela,” alieleza Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi (NNAK), Alfred Obengo jana.
Ni katika mtaa wa Kayole ambako vitendo vyake vya kutisha na vya kishetani vimegunduliwa kwenye upelelezi wa muda mrefu na mwanahabari mpekuzi wa NTV, Dennis Okari.
Taarifa hiyo inaonyesha jinsi Mugo asivyothamini maisha ya binadamu kwa kuwaweka wagonjwa wanaozuru kliniki yake kwenye hatari kubwa ya kufariki ama kupata madhara ya muda mrefu ya kiafya.
KUAVYA MIMBA
NTV ilinasa picha ambazo zinamwonyesha Mugo akiwatoa wanawake mimba kwenye kliniki yake kwa njia za kutisha, akinywa pombe kiholela anapotibu wagonjwa na kujidunga dawa ambazo hazifahamiki ni za kazi gani.
Katika kisa kimoja, alinaswa kwenye picha akimtoa mwanamke mimba, kisha kijana aliyekuwa akiomba kazi anaingia. Mugo anambiwa amwonyeshe kama kweli anajua kufanya kazi kwa kutoa sehemu za mtoto zilizokuwa zimebaki tumboni mwa mwanamke huyo.
Kijana huyo akiendelea kutoa sehemu hizo mwilini mwa mwanamke ambaye anaonekana mwenye maumivu makali, Mugo naye anaanza kumbusu na kumwambia kijana huyo kuwa hiyo ni mbinu ya kusaidia kupunguza uchungu.
Katika kisa kingine, Mugo anahudumia mgonjwa akionekana mlevi chakari, halafu anamlipisha Sh800 za dawa ambayo kwa kawaida inauzwa Sh40.
Picha hizo pia zinafichua kuwa anawatapeli wagonjwa wake. Kwa wakati mmoja, anamwitisha Sh23,000 mwanamke ambaye bintiye alifika kliniki hiyo kuavya mimba, na badala ya kumwambia ukweli anasema alikuwa akitibiwa matatizo ya tumbo.
Jana, maafisa wa kitengo cha Flying Squad walikuwa wakimsaka mwanamume huyo.
Baada ya habari hizo kufichuka, Mugo alienda mafichoni lakini akaandika kwenye moja ya akaunti zake za Facebook kuwa yule angetaka kumkamata afanye hivyo.
Waathiriwa wengi sasa wamejitokeza na kuelezea jinsi Mugo alivyowabaka, na kuavya mimba zao bila kufahamu kwao baada ya kuwadunga dawa za kuwalewesha.
Anne, ambaye si jina lake halisi ili kulinda usalama wake, anasema Mugo alitoa mimba yake bila kumfahamisha wakati alipoenda kusaka matibabu katika kliniki yake.
Anne baada ya kugundua unyama aliofanyiwa na Mugo aliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kasarani, lakini hakuna chochote daktari huyo bandia alifanyiwa licha ya maafisa wa polisi kufahamu alikokuwa.
“Mpenzi wangu alinipeleka katika kliniki hiyo mwendo wa saa tisa jioni na Mugo akasema alihitaji kufanya uchunguzi wa tumboni almaarufu ultrasound ili abaini hali ya mimba yangu ya miezi minne,” Anne alielezea Taifa Leo.
Alisema baada ya kufika katika kliniki hiyo, Mugo alimwambia sharti adungwe dawa ya ‘kupunguza uchungu’ kabla ya kuhudumiwa.
Kile hakujua ni kuwa mpenziwe alikuwa amepanga na Mugo waavye mimba yake.
Baada ya kudungwa dawa hiyo alipoteza fahamu na kurudiwa na fahamu baadaye jioni mwendo wa saa moja akiwa katika kitanda tofuati na alipokuwa amelezwa.
“Mpenzi wangu hakuwepo wakati nilipoamka. Nilipata mwanamke ambaye sikumfahamu na akanishauri nisitembee kwa sababu nilikuwa navuja damu. Mahali nilipokuwa nimelala kulikuwa kumejaa damu hali ambayo ilinishtua sana,” alielezea Anne.
Aliambiwa na mwanamke huyo kuwa mpenziwe alikuwa ameenda kumnunulia chakula cha kumpa nguvu.
KUBAKA WAGONJWA
Baada ya dakika chache Mugo alitokea na kuwaambia ametoa mimba yake kwa sababu ilikuwa inahatarisha maisha yake.
“Aliniambia kuwa baada ya kunichunguza aligundua mtoto alikuwa sehemu hatari ya tumbo na iwapo hangeavya mimba hiyo ningekufa pamoja na mtoto. Sikumuamini Mugo na baadaye niligundua walipanga njama na mpenzi wangu kwa sababu mara nyingi alikuwa amependekeza niavye mimba hiyo,” alisema Anne.
Anasema alijaribu kumtafuta mpenziwe bila kufanikiwa na baada ya kutoka kwa Mugo alienda moja kwa moja hadi katika kituo cha polisi cha Kasarani ambapo aliandikisha taarifa chini ya nambari ya OB 23/18/3/2015.
Mwathiriwa mwingine alielezea NTV kisa sawia mikononi mwa Mugo wakati alipoenda kusaka matibabu baada ya kuvuja damu kwa muda kupitia sehemu zake za siri.
“Niliona tangazo kwa jengo fulani na mwanamume niliyempata kwa simu akaniambia nitembelee kliniki yake na shida zangu za kiafya zitakuwa historia.
Alitembelea kliniki hiyo ya Mugo pamoja na mpenziwe ambaye alibaki katika eneo la mapokezi.
“Baada ya kunichunguza, Mugo aliniambia niko na uvimbe ambao ulihitaji kufanyiwa upasuaji wa haraka. Nilikuwa natetemeka na nikamuomba anipe nakala ya ripoti ya uvimbe huo ili niende nisake ushauri zaidi kabla ya upasuaji,” akaeleza.
Mugo alisisitiza kuwa afanyiwe uchunguzi zaidi kabla ya kwenda ilia pate ripoti kamili kuhusu uvimbe huo. “Aliniambia nifungue mdomo na akaniweka tembe tatu za dawa chini ya ulimi. Nilipoamka nilijipata kitandani nikiwa nimeloa damu huku mpenzi wangu akipiga nduru. Sikuwa na nguo zangu za ndani na ilikuwa wazi kuwa nilibakwa,” alielezea mwanamke huyo.
Mugo alikamatwa mnamo 2015, kuhusiana na tuhuma za kudhulumu wagonjwa katika kliniki yake ya Githurai 44. Hata hivyo, kesi hiyo ilisambaratika 2016 baada ya mashahidi na waathiriwa kukosa kuandikisha taarifa ambazo zingetumika dhidi yake.
KLINIKI NYINGINE
Wakazi wa Kayole waliambia Taifa Leo kuwa Mugo alifungua kliniki nyingine kwa jina ‘Ultrasound Centre’ karibu na nyumba za kukodisha eneo la Choma Villas, lakini alikuwa anaonekana akisafirisha wanawake waliozirai katika kliniki iliyokuwa karibu kwa jina Millan Medical Centre.
“Sijui nini hufanyika katika kliniki hiyo lakini nimekuwa nikiwaonya wanawake dhidi ya kusaka matibabu kwa Mugo,” alisema Joyce Mengesa, mhudumu wa Salon karibu na kliniki hiyo.
Bi Mengesa alisema Mugo anafahamika vyema kwa kuwapotezea wanawake fahamu hata wakati hawahitaji kufanyiwa upasuaji.
Mkuu wa Kitengo cha Ujasusi (DCI) George Kinoti aliambia Taifa Leo kuwa ametuma kikosi kikubwa cha maafisa ambao wamepewa maagizo ya kumkamata.
Mugo alifuzu kwa digrii ya Sayansi katika Uuguzi (Bachelor of Nursing) kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi mnao 2000. Hata hivyo, hajasajiliwa kama daktari na Bodi ya Madaktari.