Habari

Murkomen alia ukahaba unarejesha nyuma jiji la Eldoret

Na TITUS OMINDE July 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen ametaja ukahaba ambao ni biashara ya tangu jadi kuwa miongoni mwa sakata ambazo zimekumba jiji la Eldoret na maeneo mengine ya North Rift.

Akihutubia wanahabari pembeni mwa kikao cha Jukwaa la Usalama, Bw Murkomen alijutia kuwa walaghai wengi hutumia visivyo ukarimu wa wenyeji ndio maana visa vya sakata mbalimbali ikiwemo ukahaba vinazidi kuongezeka kila uchao katika jiji la Eldoret.

Bw Murkomen alisababisha kicheko alipotaja ukahaba kuwa miongoni mwa sakata ambazo zinatatiza wenyeji wa jiji hilo la tano nchini.

“Eldoret ni jiji lenye utajiri mwingi ndio maana watu wengi wanatumia hali hiyo kushiriki ulaghai mbali mbali ikiwemo sakata ya ajira ughaibuni, masomo pomoja na ile biashara ya tangu jadi ambapo wanawake wanatumia nafasi hiyo hasa msimu wa kuvuna kulaghai wanaume pesa zao walizozipata kwa jasho,” alisema Bw Murkomen huku washiriki wakiangua kicheko.

Waziri huyo aliwataka wakaazi wa maeneo hayo kuwa macho ili kujiepusha na walaghai ambao wamevamia jiji hilo.

Hata hivyo, aliwataka maafisa wa usalama kuimarisha msako dhidi ya walaghai na kuhakikisha kuwa wamefikisha mahakamani.

Kuhusu uchunguzi unaoendelea wa ulanguzi wa viungo ambapo hospitali ya Mediheal jijini humo inahusisha na sakata hiyo, Bw Murkomen alielezea matumaini ya ukweli kuhusu sakata hiyo kupatikana baada ya uchunguzi kukamilika.

Waziri huyo alitaja sakata hiyo kuwa miongoni mwa sakata ambazo zinaletea jiji hilo sifa mbaya.

“Tusiingilie suala hilo la ulanguzi wa viungo linalofungamana na hospitali ya Mediheal kuhusu sakata ya biashara ya viungo ambalo limo mikononi mwa waziri mwenzangu, hata hivyo ulanguzi huo ni miongoni mwa sakata ambazo zifanya Eldoret kuwa kitovu cha sakata na ulaghai,

“Hapa ndiko kuna sakata ya masomo, ajira ughaibuni, mashamba miongoni mwa sakata nyingine. Kwa sasa uchunguzi kuhusu sakta ya viungo unaendelea na hivi karibuni wahusika watakbiliwa kisheria,” alisema Bw Murkomen.

Jiji la Eldoret limekuwa maarufu kwa sakata na ulaghai mbalimblai huku vitengo vya usalama vikimulikwa kuhusiana na kuenea kwa sakata hizo.