Muturi aagiza wabunge kuwaadhibu mawaziri wanaokosa kufika mbele yao
Na CHARLES WASONGA
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameziagiza kamati mbalimbali kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri ambao watafeli kufika mbele yazo kujibu maswali na masuala yanayohusu wizara zao.
Hatua hiyo ni pamoja na kuanzisha mchakato wa kuwaondoa mamlakani kulingana na uwezo ambao bunge limepewa kwenye kipengee cha 152 (6) cha Katiba ya sasa.
“Mawaziri wakikosa kuwajibikia majukumu yao ambapo wanakosa kufika mbele ya kamati mbalimbali za bunge kujibu maswali kutoka kwa wabunge, kamati husika zinafaa kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuanzisha mchakato wa kuwaondoa afisini,” akasema Bw Muturi mnamo Jumanne alasiri.
Akaongeza: “Na ikiwa mawaziri hao watawatuma mawaziri wasaidizi (CASs) ambao hawana ufahamu kuhusu masuala ambayo wabunge wanataka yafafanuliwe, muwafukuze. Hii ni kwa sababu hamuwezi kusikiza mtu ambaye hawezi kuwahakikishia kuwa anayoyasema yanawakilisha msimamo rasmi wa wizara zao.”
Bw Muturi alionekana akimrejelea Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ambaye Jumanne asubuhi alifeli kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Usalama kujibu jumla ya maswali 14 kutoka kwa wabunge.
Maswali hayo yalihusu masuala yanayofungamana na majukumu ya wizara yake; mathalan utovu wa usalama katika sehemu mbalimbali nchini.
Badala yake Dkt Matiang’I alimtuma Waziri Msaidizi katika Wizara hiyo Patrick Ole Ntutu kumwakilisha lakini wanachama wa Kamati hiyo wakiongozwa na naibu mwenyekiti John Waluke wakamfurusha.
Bw Ntutu alijaribu kuelezea Kamati hiyo kwamba afisi ya Spika au makarani wa kamati hiyo hawajaiandikia Wizara yake ikitoa agizo kwamba hafai kumwakilisha Waziri Matiang’I bungeni, lakani wabunge hao walikataa kusikia maelezo yake.
“Wewe rejea afisini umwambia Matiang’I kwamba tunamtaka afike mbele ya kamati hii Jumanne wiki ujao bila kuchelewa. Hatutambui wadhifa wako kwa sababu hautambuliwi katika katiba ya sasa,” akasema Bw Waluke ambaye ni Mbunge wa Sirisia.
Mwaka jana, Bw Muturi aliwaagiza wabunge kuwalazimisha mawaziri kuwajibika kwa majibu wanayotoa mbele ya kamati zao. Vile vile, aliambia Kamati ya Utekelezaji kufuatilia majibu yanayotolewa na mawaziri na kuhakikisha kuwa yanaakisi uhalisia wa mambo mashinani.