Habari

Muturi, balozi McCater watofautiana kuhusu kujitolea kwa Amerika kuukabili ugaidi

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Balozi wa Amerika nchini Kyle McCater wametofautiana kuhusu suala la kujitolea kwa taifa hilo lenye nguvu duniani katika vita dhidi ya ugaidi.

Kulingana Bw Muturi kundi la al-Shabaab limekuwa likipokea ufadhili kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kigeni kwa sababu kufikia sasa “Amerika haijalitangaza rasmi kuwa kundi la kigaidi.”

“Kwa sababu kufikia sasa Amerika haijatoa msimamo wake rasmi kwamba al-Shabaab ni kundi la kigaidi, ndiposa limeendelea kusawiriwa kama kundi la kijamii nchini Somalia. Na hivyo, linapokea misaada ya kifedha kutoka kwa mashirika ya kimataifa,” akasema Bw Muturi alipohutubu katika ukumbi wa KICC, Nairobi.

Akaongeza: “Ufadhili kwa kundi hili na makundi mengine ya wahalifu unapaswa kuzimwa ili ulimwengu uweze kushinda vita dhidi ya ugaidi.”

Hata hivyo, dai hilo la Bw Muturi lilipingwa na Bw McCater aliyejibu kuwa Amerika haijafeli kutangaza al-Shabaab kama kundi la kigaidi.

“Amerika iliunga mkono azimio nambari 751 la Umoja wa Mataifa (UN) ambalo linashikilia kuwa al-Shabaab ni kundi la kigaidi ambalo ulimwengu mzima unafaa kupambana nalo kwa kuwa ni tishio la usalama,” akasema.

Kongamano

Wawili hao walikuwa wakiongea wakati wa kongamano la kimataifa la wabunge kuhusu mikakati kupambana na uhalifu wa kimataifa.

Bw McCater alisema Amerika imekuwa ikifadhili juhudi za Kenya katika vita dhidi ya ugaidi kwa kiasi cha zaidi ya dola 100 milioni (Sh10 bilioni) kila mwaka, hatua inayoashiria kujitolea kwake kufanikisha vita hivyo.

“Hakuna tashwishi kwamba Amerika iko mstari wa mbele katika suala hili. Na tuna matumaini kuwa ulimwengu utashinda vita dhidi ya uhalifu huo,” akakariri.

Hata hivyo, Bw McCater alisema Amerika haijafurahishwa na tangazo lililotolewa na serikali ya Kenya kwamba huenda ikakata misaada ya kibinadamu kwa taifa la Somalia.

“Kenya inapaswa kuweka kando mpango huo kwa sababu utahujumu vita dhidi ya ugaidi,” akasema.

Mkutano huo unaoshirikisha wabunge na wataalamu mbalimbali katika nyanja ya usalama pia unajadili uhalifu wa kimtandao, ulanguzi wa fedha, ulanguzi wa dawa za kulevya, ufisadi miongoni mwa aina nyingine za uhalifu.

Wabunge wanajadili namna wanavyoweza kushirikiana na asasi husika za serikali kubuni sheria na sera wezeshi za kupambana na uhalifu.

Wajumbe wanaohudhuria mkutano huo, utakaotamatika Jumanne, wanatoka mataifa kama vile Amerika, Uingereza, Italia, Brazil, Ethiopia, Zimbabwe, Djibouti miongoni mwa mengine.