Mwaka mmoja baada ya Wamakonde kutambuliwa, bado ni kilio
KAZUNGU SAMUEL na FADHILI FREDRICK
Kwa ufupi:
- Wamakonde walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru
- Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho
- Sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa 2017 na Rais Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa tena
- Wanalia kuwa kumiliki ardhi kwao ni tatizo kuu huku wakitengwa na majirani zao licha ya kukubaliwa kama kabila la 43 nchini
MWAKA mmoja si kipindi kirefu katika maisha ya kawaida, hawa iwapo katika muda huo, mtu anasubiri kutimiziwa ahadi fulani.
Kauli hii ni sahihi zaidi kwa watu wa kabila dogo kutoka taifa la Msumbiji, ambao juhudi zao za kutaka kutambuliwa zilizaa matunda mwaka jana, wakati wa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Jamii ya Wamakonde, ambao walifika katika kaunti ya Kwale miaka michache baada ya Kenya kujinyakulia Uhuru, ilijikuta ikiendelea kuzaana na kujazana katika kijiji cha Makongeni, kando mwa barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga, katika kaunti ya Kwale.
Taifa Leo ilipowatembelea wakazi hao mwaka mmoja tangu watambuliwe kuwa kabila la 43 la Kenya, wakazi wa kabila hilo walikuwa wengi wa matumaini kwamba labda walikuwa wamefikishiwa habari njema.
Kijiji hicho ambacho hakikuonekana kuwa na shughuli nyingi, ndiyo makao ya jamii hiyo ya Wamakonde.
Wamekuwa wakifanya kazi katika mashamba ya makonge na sukari maeneo ya Msambweni na Ramisi mtawalia lakini walijikuta wakiwa na changamoto nyingi, hasa ile ya kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa, ambavyo vingewasaidia kupewa vitambulisho.
Ingawa wamekuwa wakisoma katika shule za Kenya na kupata elimu na ujuzi, safari yao imekuwa ikifikia darasa la nane au kidato cha nne, kwa kuwa baada ya hapo wamekuwa hawapati ajira kwa vile hawakuwa na vitambulisho vya kitaifa.
Katikati ya kijiji hiki kuna kibao chenye ujumbe unaosema hivi ‘Kama kumbukumbu ya kukumbuka jamii ya Wamakonde ambao walikuja Kenya kama wafanyikazi katika mashamba ya makonge. Jamii hii ilipewa rasmi uraia wa Kenya mwaka wa 2016,’ kinasema kibao hicho.
Hata hivyo, sherehe ya kuitambua jamii hiyo kuwa sehemu ya makabila ya Kenya, ilifanywa mwaka jana Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa kwenye kampeni zake za kutaka kuchaguliwa kwa kipindi cha pili cha uongozi.
Kuna mti kando ya kibao hicho ambao ulipandwa siku ambapo jamii hiyo iliidhinishwa na serikali kuwa mojawapo ya jamii za Kenya.
Matumaini
Kwa hivyo, baada ya kutambuliwa, kulikuwa na matumaini makubwa kwamba sasa Wamakonde wangenufaika na miradi na mambo mengine ambayo jirani zao Wadigo na Wakamba wamekuwa wakinufaika nayo.
Hata hivyo msemaji wa jamii hiyo, Bw Thomas Nguli, anasema kuwa Wamakonde hawajaona yale matunda waliyokuwa wakitarajia kupata, ambayo yalifaa kuandamana na wao kufahamika rasmi Wakenya.
“Tunashukuru kwamba kwa sasa sisi ni Wakenya lakini bado tuko na changamoto nyingi ambazo zinatuathiri kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano sasa hivi sisi hatuna mashamba wala ardhi. Hatuna hati miliki za kijiji hiki ambacho sisi tumepaita nyumbani kwa miaka mingi,” akasema Mzee Nguli.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa jamii hiyo kwa sasa iko na zaidi ya watu 1,000 ambao wamepata vitambulisho vya kitaifa.
“Tunamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kutuwezesha kupata uraia wa taifa hili, lakini hatuwezi kusema kwamba tumepata uhuru wetu wakati ambapo bado tunatatizika kumiliki ardhi. Hii ni shida kubwa,” akasema Mzee Nguli.
Kutengwa
Alisema kuwa changamoto nyengine ambayo inawakabili ni kutengwa na majirani zao na hilo halijakuwa jambo jema kwao.
“Hapa wanatuita watoto wa Uhuru lakini tungeomba tu kama majirani zetu wanaweza kutambua kwamba sisi sasa ni Wakenya kama wao na wanafaa kututambua,” akasema Mzee Nguli.
Aliongeza kwamba jumla ya wakazi 1,875 kutoka kwa jamii hiyo tayari wamepata vitambulisho na hata wengine wakijisajili kama wapiga kura katika kaunti hiyo.
“Kutokana na mateso mengi tuliyopitia kama watu tusio na makao katika nchi hii ambayo tumeishi maisha yetu yote, tunadhani kwamba matakwa yetu sharti yaangaliwe kikamilifu na suluhisho la kudumu lipatikane,” akasema Bw Nguli.
Tutalala tu na amani ikiwa tutahakikishiwa kuajiriwa na serikali na kila aina ya jambo ambalo litatuwezesha kimaisha,” akaongeza.
Kupata kazi za serikali
Alisema kuwa kutambuliwa kwao hata hivyo kumewapatia faida kiasi kwani kuna watu sita miongoni wao ambao wamepata kazi baada ya kupewa uraia.
“Tuko na vijana wawili ambao wamejiunga na idara ya huduma za polisi na wane wameingia katika idara ya magereza. Zaidi ya vijana 200 sasa wameingia katika mradi wa huduma kwa taifa (NYS),” akasema Mzee Nguli.
Kulingana na Rose Boniface aliye na umri wa miaka 50, ilikuwa furaha kuu baada ya kupata kitambulsho tangu azaliwe. Hatua hiyo alisema ilimwezesha kushiriki katika uchaguzi wa wa mwaka 2017.
Alisema kabla ya kupata stakabadhi hiyo muhimu, maisha yalikuwa yamejaa usumbufu kwa vile hakuweza kupata huduma muhimu katika ofisi ya umma na vile vile alikuwa mara nyingi akisumbuliwa na polisi.
“Ilikuwa ni vigumu sana na tuliteseka sana miongoni mwetu ila sasa hali ni tofauti,” akasema.
Aliongeza kwamba mradi muhimu kama vile malipo kwa wazee walikuwa hawapati lakini sasa wamewekwa kaitka mpango huo.
Julieta Simenya, katibu wa kundi hilo alisema kuwa jamii bado inapitia changamoto kadhaa ambazo bila kuangaliwa vyema, zitatizika.
Kumiliki ardhi
“Shida yetu kuu ilikuwa ni kupata uraia wa Kenya lakini pia tulikuwa na nyengine kama vile umiliki wa mashamba. Kwa sababu sasa tumepata vyeti vya kuzaliwa na kuwa raia kamili, serikali sasa haina budi kuangalia jinsi ambavyo itatusaidia tupate mashamba,” akasema Bi Simenya.
Jamii hiyo ina ukoo kutoka nchini Msumbuji na walikuja Kenya kupitia Tanzania Kusini ili kuja na kufanya kazi katika mashamba ya Makonge katika kaunti za Kwale na Kilifi.
Hata hivyo jamii hizo zilikumbana na hali ngumu baada ya kampuni za miwa na makonge kufilisika ambapo walijikuta wakiosa mahali pa kwenda.
Baada ya miaka mingi ya kutengwa, Bw Nguli alisema kuwa kwa kushirikiana na mashirika ya haki za kibinadamu, serikali iliwapatia uraia mwaka wa 2016.
“Tulianza safari hii mwaka wa 1995 na mimi sasa hata nikifa nitakuwa na furaha kwamba nilifanya kazi uyangu kubwa ya kufikisha watu wangu mahali walipotamani,” akasema Mzee Nguli.