HabariSiasa

Mwana mpotevu atarudi nyumbani?

August 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Jumanne alikutana na kinara mwenza wa NASA, Moses Wetangula, katika juhudi za kumshawishi asihame muungano huo wa upinzani.

Wawili hao walikutana katika afisi za chama cha Wiper mtaani Karen jijini Nairobi siku tatu baada ya Bw Musyoka kuahidi kuwa atampatanisha kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ili kuokoa NASA.

Bw Wetangula amekuwa akimshambulia Bw Odinga tangu chama cha ODM kilipompokonya wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti siku chache baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kujiapisha kuwa rais wa wananchi Januari 30.

Bw Wetangula, Bw Musyoka na kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi, walisusia hafla ya kumuapisha Bw Odinga katika bustani ya Uhuru Park jijini Nairobi.

Tofauti za Bw Wetangula na Bw Odinga zilizidi kiongozi huyo wa ODM alipoacha vinara wenza wa NASA katika mazungumzo yake na Rais Kenyatta.

Alitangaza kuwa muungano wa NASA ulikufa na umebaki gofu akisisitiza kuwa, hatashirikiana kisiasa na Raila japo Bw Musyoka na Bw Mudavadi wanasisitiza muungano ungali imara.

“Ndoa yangu na Bw Raila imekufa. Ni mwanasaisa anayetumia watu na kuwatupa. Tunajua alikuwa Kanu, akaibomoa, tulikuwa naye Narc, akaivunja, tukaunda Cord akaibomoa pia na sasa amevunja NASA,” alisema alipohojiwa na runinga ya Citizen wiki moja lililopita.

Wanasiasa wa chama cha ODM wamekuwa wakimkashifu Bw Wetangula wakimtaka aondoe wabunge wa chama chake kutoka kamati za bunge iwapo amehama NASA.

Bw Kalonzo ambaye alikuwa ng’ambo uhasama kati ya Wetangula na Raila ulipozidi, aliahidi kuwapatanisha.

Jana, duru katika Wiper zilisema kwamba, Bw Musyoka aliahidi kuendelea kuwa gundi inayounganisha muungano huo na kwamba, hatalegeza juhudi za kuhakikisha vinara wenzake wanazungumza kwa ustawi na amani nchini.

Kwenye taarifa, chama hicho kilisema Bw Wetangula alipongeza Wiper kwa kufungua ofisi mpya mtaani Karen.

“Vyama vya Ford-Kenya na Wiper vina malengo sawa ya siku zijazo kuhusu nchi hii , tutaendelea kujitolea na kuungana,” taarifa ilisema ikinukuu Bw Wetangula alivyoandika katika kitabu cha wageni katika ofisi za Wiper.

Kwenye anwani yake ya Twitter, chama hicho kilipakia picha za Bw Wetangula akitabasamu huku akisalimiana na Bw Musyoka.

Wakenya wanasubiri kuona iwapo juhudi za Bw Musyoka kufufua NASA zitafaulu kwa sababu Bw Wetangula alinukuliwa akiapa kutoshirikiana tena na Bw Raila.

Chama cha Wiper kimetangaza kuwa kitashirikiana na chama cha Jubilee sawa na ODM cha Bw Raila, huku Bw Wetangula akijitangaza kiongozi rasmi wa upinzani. Duru zinasema Bw Musyoka anafanya juhudi za kukutanisha vinara wote wa NASA waweze kuzika tofauti zao.