Habari

Mwanaharakati Agather aliyekamatwa pamoja na Bonface Mwangi, aachiliwa huru

Na WINNIE ONYANDO May 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAHARAKATI mwingine aliyekuwa akizuiliwa Tanzania ameachiliwa huru.

Agather Atuhaire ambaye pia ni wakili na mwanahabari alipatikana eneo la Mutukula kwenye mpaka wa Tanzania na Uganda.

Habari za kuachiliwa kwake zilisambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa X na Godwin Toko ambaye pia ni naibu wa timu ya Agora.

“Hatimaye Agather ameachiliwa huru. Nimezungumza naye kupitia simu ya dadake. Aliachiliwa kwenye mpaka wa Uganda na Tanzania,” alisema Bw Toko.

Mwanaharakati huyo alikuwa akizuiliwa pamoja na Boniface Mwangi wa Kenya aliyeachiliwa huru jana.

Mwanaharakati huyo alikuwa hajulikani aliko kwa siku kadhaa baada ya kukamatwa wiki hii nchini Tanzania.

Boniface Mwangi alirejeshwa nchini kwa barabara Alhamisi kabla ya kupatikana akiwa ametupwa Ukunda, Kaunti ya Kilifi. Katika mkutano na waandishi wa habari, Mwangi alisema waliteswa pamoja na Agather, huku akitoa wito wa kuachiliwa kwake.

Mwanaharakati Hussein Khalid, Mkurugenzi Mtendaji wa VOCAL Africa, alithibitisha kuachiliwa kwa Agather, akisema kuwa hali yake si nzuri na akatoa wito wa haki kutendeka kwa wanaharakati hao.

 “Ameteswa, amejeruhiwa, mwili umevunjika lakini roho ni thabiti. Agather amepatikana. Lazima wawajibike kwa waliyomtendea Boniface Mwangi na Agather. Haki lazima itendeke na ionekane kutendeka,” alisema Khalid.

Agather na Mwangi walikamatwa jijini Dar es Salaam Mei 19 walipokuwa wakihudhuria kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu.

Familia ya Agather ilithibitisha kuwa alipatikana akiwa ametupwa eneo la mpakani  Mutukula usiku. Hali halisi ya kuachiliwa kwake haijafahamika wazi, na bado hajatoa tamko lolote kwa umma.

Kukamatwa kwao kuliibua hisia kali kimataifa, huku mashirika ya haki za binadamu yakitoa wito wa kuheshimiwa kwa haki za wanaharakati.

Mapema wiki hii, Rais Samia Suluhu alionya wanaharakati wa kigeni dhidi ya kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.