Habari

Mwanamke ang’ang’ania mali ya mwanajeshi

Na JOSEPH OPENDA April 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAMKE mmoja anapigania udhibiti wa mali ya afisa mkuu wa kijeshi ambaye alikufa mwaka jana baada ya uchunguzi wa DNA kuthibitisha kuwa marehemu ni baba wa mtoto wake.

Kanali Flavian Mwangi, ambaye alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Mafunzo cha Wanahewa nchini alipatikana amefariki ndani ya gari lake muda mfupi baada ya kuondoka kambini saa kumi jioni mnamo Septemba 26, 2024.

Kifo chake kilizua mzozo wa mali yake baada ya mwanamke kujitokeza akidai kuwa alikuwa mke wake wa pili wa marehemu kwa sababu ana mtoto wake wa miaka saba.

Ghasia zilitanda wakati wa mazishi ya Kanali Mwangi mwanamke huyo akimshutumu mjane, mama wa watoto watatu kwa kumtenga mwanawe katika mipango ya mazishi.

Mwanamke huyo alifaulu kushawishi mahakama kuamuru uchunguzi wa DNA kuthibitisha ikiwa marehemu alikuwa baba wa mtoto wake.

Matokeo ya DNA yaliyotolewa mnamo Desemba 30, 2024 yalithibitisha kuwa mwanawe alikuwa mtoto wa marehemu.

Kufuatia kudhibitishwa kwa ripoti ya DNA na Hakimu Mkuu G.M. Gitonga mnamo Februari 11, 2025, mwanamke huyo aliwasilisha ombi jipya akitaka mapato yote ya fedha ambayo ni sehemu ya mali ya Kanali Mwangi kuwekwa kwenye akaunti tofauti hadi kesi ya urithi isikizwe.

Mwanamke huyo alitaka mahakama imruhusu arithi sehemu ya mali ya marehemu kwa manufaa ya mwanawe.

Anataka wasimamizi wa sasa walazimishwe kutoa mahitaji ya haraka ya mtoto ikiwa ni pamoja na karo ya shule, usafiri, kodi ya nyumba, gharama za maisha na pesa ya kulipa madeni.

Katika hati yake ya kiapo, alisema kwamba Kanali Mwangi alimsaidia mtoto huyo akiwa hai lakini msaada huo ulikatika baada ya kifo chake, ikidaiwa ni kwa sababu mjane huyo aliingilia kati.

Anadai mwanawe ameachwa akiteseka huku watoto wengine wakiishi maisha mazuri.