Mwanasheria Mkuu mpya mtarajiwa aahidi kutatua janga la ufisadi nchini
Na LUCY KILALO
Kwa ufupi:
- Jaji Kariuki aahidi kukabiliana na ufisadi akisema kuwa atafanya vikao na afisi husika kubainisha changamoto za vita dhidi ya ufisadi
- Sijawahi kutuhumiwa kwa ufisadi, kushindwa kutekeleza kazi ama kushawishiwa kwa njia yoyote nyingine. Nguvu yangu inatokana na tajriba yangu, amesema
- Aahidi kufuatilia suala la kurejesha mali iliyopatikana kutokana na ufisadi na kubainisha chanzo cha baadhi ya mawakili wanaowakilisha serikali kudai kiasi kikubwa cha pesa
- Awahakikishia Wakenya kuwa katika utendakazi wake, atafuata Katiba na hataegema upande wowote wa kisiasa
JAJI Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa kwa nafasi ya Mwanasheria Mkuu Alhamisi ameahidi kudumisha Katiba na Sheria za nchi na kuishauri serikali vilivyo, bila kushawishiwa kisiasa ama kwa njia nyingine yoyote.
Jaji Kariuki ambaye amekuwa Rais wa Mahakama ya Rufaa alikuwa mbele ya Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa, inayoongozwa na Spika Justin Muturi, kupigwa msasa alielezea misimamo yake kuchangiwa zaidi na malezi yake, dini katika kanisa la Kianglikana pamoja na kuthamini utekelezaji wa haki.
“Ikiwa nitaidhinishwa, ninawahakikishia kuwa nitaelekezwa na Katiba. Afisi ya Mwanasheria Mkuu inawakilisha watu wa Kenya na sio chombo cha chama chochote cha kisiasa,” alisema.
Jaji Kariuki pia aliahidi kukabiliana na ufisadi akisema kuwa atafanya vikao na afisi nyingine husika kama ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Idara ya Upelelezi (DCI) na hata Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) kuweza kubainisha changamoto ziko wapi, kuhusiana na kesi za ufisadi.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Adan Duale alitaka kujua kwa nini katika miaka michache iliyopita, uhusiano baina ya urais, bunge na mahakama haujakuwa wa kuridhisha, huku akimtaka aeleze ikiwa mtangulizi wake alishindwa na kazi.
Akijibu, Jaji Kihara alisema haitakuwa vyema kumjadili mwenzake, ingawa alikiri kuwepo kwa mivutano hiyo, na kuahidi kubadilisha hali hiyo.
Daraja la mazungumzo
“Lazima tufanye kazi pamoja. Lazima tuongee, kwani hiyo ndiyo njia ya pekee ya kupatia katiba nafasi, kibinafsi na kwa pamoja. Afisi ya Mwanasheria Mkuu inaweza kuwa daraja la mazungumzo kwa pande hizo tatu.”
Wakati huo huo, Jaji Kihara alijitetea kuhusiana na kesi ambayo mahakama ya Rufaa ilidaiwa kufanya kikao usiku na kubatilisha uamuzi uliokuwa umetolewa na Mahakama Kuu wakati wa uchaguzi 2017.
Alisema wajibu wake kama rais ulikuwa wa kuunda kikao kitakachosikiza kesi pekee, hata hivyo hangetoa maelezo zaidi kwa kuwa alihojiwa na Tume ya Idara za Mahakama (JSC), na aliwasilisha majibu yake, na anachosubiri ni uamuzi wa tume hiyo.
“Sijawahi kutuhumiwa kwa ufisadi, kushindwa kutekeleza kazi ama kushawishiwa kwa njia yoyote nyingine. Nguvu yangu inatokana na tajriba yangu na kwamba haki lazima itekelezwe.’
“Sitatingishwa kufanya kile kinachoenda kinyume na Katiba na Sheria.”
Pia alitetea uamuzi wake wa kukubali uteuzi huo baada ya Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma ambaye bali na kumsifia utendaji kazi wake akiwa mahakamani, alishangaa kwa nini akubali nafasi ambayo itamnyima amani.
Jaji Kariuki alisema lengo lake ni kutumikia nchi yake, akieleza kuwa hata akiwa jaji amekabiliwa na shinikizo nyingi.
Uaminifu
“Kubadilisha nchi hii, lazima tupate wanawake na wanaume ambao ni waaminifu tayari kutumikia nchi yao,” alisema akiongeza kuwa hakuna haja kwa mtu “kuupata ulimwengu wote lakini kuiuza nafsi yake.”
Vile vile, aliahidi kufuatilia suala la kurejesha mali iliyopatikana kutokana na ufisadi na kubainisha chanzo cha baadhi ya mawakili wanaowakilisha serikali kudai kiasi kikubwa cha pesa, baada ya Spika Muturi kuzua hofu kuwa huenda ni njama nyingine ya kufuja pesa kutoka kwa serikali.
Jaji Kariuki ambaye aliwasifia wazazi wake na mkewe kuweza kufikia mahali alipo, alieleza kuwa alikuzwa kuthamini Wakenya kama watu wanaoamini ukweli na haki.
Akitoa mfano wa jinsi ua linalovyochanuka na mwishowe urembo wake kubainika, ndivyo kila Mkenya anafaa ajaribu kuona uzuri kwa mwenzie ili kukuza utaifa.