Mwili wa mwanamume waopolewa, watambuliwa kuwa wa John Mutinda
MOHAMED AHMED Na WACHIRA MWANGI
MWILI wa mwanamume umeopolewa na mpigambizi wa jeshi la wanamaji – Kenya Navy – katika kivuko cha Likoni ambapo gari limedondoka kwenye feri Jumamosi saa kumi na dakika ishirini (4:20a.m.) na kutumbukia katika Bahari Hindi.
Mwanamume huyo ametambulika kama John Mutinda aliyekuwa na umri wa miaka 46. Nambari ya usajili ya gari lake ni KBX 475B na lilikuwa aina ya Toyota Allion na lenye rangi nyekundu.
Feri tano ambazo zimekuwa zikitoa huduma za usafiri zipo majini lakini shughuli zao zimesitishwa zingatio likiwekwa katika uokozi na uopoaji.
Gari dogo aina ya Saloon limetumbukia baharini likiwa na idadi ya watu ambayo haijabainika wazi, kulingana na Shirika la Huduma za Feri nchini (KFS).
Tayari Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Hassan Joho ametuma salamu za pole mara baada ya kutokea mkasa huo wa Likoni.
Bw Joho amesema Jumamosi kwamba ametuma wapigambizi kutoka kwa ofisi yake kusaidia katika uokozi.
“Nawataka watumiaji wa feri wawe makini kuepukana na maafa ambayo yanaanza kuwa mazoea,” amesema gavana Joho kwenye taarifa.
Hii si mara ya kwanza mkasa kama huu kutokea katika kivuko cha Likoni.
Mwanamke na mwanawe walizama katika kivuko hicho Septemba 29, 2019.
Maiti za marehemu Mariam Kighenda aliyekuwa na umri wa miaka 35 na mwanawe Amanda Mutheu ziliopolewa baada ya miili yao kukaa ndani ya bahari kwa muda wa siku 13.