Mwili wa Raila hautalala kwake Karen kabla ya kusafirishwa Kisumu – ODM chatangaza
CHAMA cha ODM kimetangaza mabadiliko katika mpango wa mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, kikitaja sababu za kiusafiri ambazo haziwezi kuepukwa.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano Philip Etale alisema mwili wa mwendazake hautapelekwa nyumbani kwake Karen kukesha kama ilivyopangwa awali.
“Baada ya shughuli ya kutazama mwili inayoendelea wakati huu katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo, utarejeshwa katika hifadhi ya Lee kutayarishwa kabla ya kusafirishwa kwa ndege hadi Kisumu kesho asubuhi,” taarifa hiyo ikasema.
Kulingana na mpango wa awali, mwili wa Raila ulitarajiwa kukesha nyumbani kwake baada ya maafisa wakuu kuutazama katika majengo ya Bunge na raia kuutazama katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo.
Kulingana na mila na tamaduni za jamii ya Waluo, maiti ya Mzee wa hadhi ya Raila sharti ilazwe nyumbani kwake kabla ya kusafirishwa kwa mazishi.
Lakini, Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Mazishi ya Raila inayoongozwa kwa pamoja na Naibu Rais Kithure Kindiki na Seneta wa Siaya Oburu Oginga, ilibadilisha mipango hiyo ili kutoa nafasi ya utayarishaji wa miwili kabla ya kusafirishwa hadi Kisumu Jumamosi, Oktoba 18, 2025.
Mjini Kisumu, ibada ya ukumbusho itafanyika katika Uwanja wa Michezo wa Jomo Kenyatta, mtaa wa Mamboleo.
Viongozi wa ukanda wa Nyanza na Magharibi mwa Kenya wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo. Baadaye, umma utapewa nafasi ya kuutazama mwili huu kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo aliyehusudiwa pakubwa katika eneo hilo.
Baadaye, mwili utasafirishwa kwa barabara hadi nyumbani kwake Opoda Farm, Bondo, kaunti ya Siaya.
Raila atazimwa Jumapili, Oktoba 19, 2025 nyumbani kwa babake, Kang’o Kajaramogi, kando ya kaburi la Jaramogi Oginga Odinga.