Nairobi, Pwani zafungwa
Na BENSON MATHEKA
SERIKALI Jumatatu ilitangaza kuwafungia mahala waliko wakazi wa maeneo yaliyo na visa vingi vya virusi vya corona.
Rais Uhuru Kenyatta alitaja hatua hiyo kuwa inayokusudiwa kuwazuia watu wanaoishi Nairobi na viunga vyake, Mombasa, Kwale na Kilifi kusambaza ugonjwa huo maeneo mengine ya nchi.
Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa vingi vya maambukizi kwa asilimia 82 huku Mombasa, Kilifi na Kwale zikiwa na asilimia 14 kwa jumla.
Hapo jana, idadi ya walioambukizwa iliongezeka hadi 158 baada ya watu wengine 16 kuthibitishwa wanaugua.
Kulingana na agizo la serikali, hakuna mtu yeyote kwa kutumia baiskeli, bodaboda, tuktuk, gari, chombo cha bahari, treni ama ndege atakayeruhusiwa kuingia ama kutoka Nairobi na viunga vyake, Kilifi, Kwale na Mombasa kwa siku 21 zijazo.
Rais alifafanua kuwa usafiri ndani ya Nairobi na viunga vyake, kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa utaendelea kulingana na kanuni za kafyu iliyotangazwa awali.
“Usafiri ndani ya Nairobi na kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa utaendelea lakini usafiri wa kuingia na kutoka hautaruhusiwa,” akasema Rais Kenyatta.
Hii ina maana kuwa shughuli za kawaida zitaendelea lakini watu watahitajika kuzingatia kanuni za kunawa mikono, kutokaribiana na kufunika midomo na mapua kwa vitambaa wanapokuwa nje ya nyumba.
Alifafanua kuwa Nairobi na viunga vyake inajumuisha Kaunti ya Kiambu hadi Daraja la Chania mjini Thika, Rironi, Ndenderu na Kiambu mjini; Kaunti ya Machakos hadi Katani na Kaunti ya Kajiado hadi Kitengela, Kiserian, Ongata Rongai na Ngong mjini
Rais Kenyatta alisema marufuku ya kuingia na kutoka Nairobi yaanze saa moja jana usiku na marufuku sawa katika kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale kuanzia Jumatano wiki ijayo.
Polisi wameagizwa kuhakikisha hakuna magari, baiskeli, pikipiki, skuta, gari moshi, ndege, mashua au meli zitakazosafirisha watu kuingia na kutoka maeneo hayo.
Rais alisema magari yanayosafirisha chakula na bidhaa tofauti hayatazuiwa lakini lazima yawe na dereva na wasaidizi walioidhinishwa na mwenye gari kwa maandishi na kupatiwa vibali na serikali.
“Safari za magari ya kubeba chakula na bidhaa nyingine zitaendelea kama kawaida wakati wa kipindi hiki kupitia barabara, reli na ndege. Gari lolote la kubeba mizigo litakuwa na dereva mmoja pekee na wasaidizi walioruhusiwa kwa barua kutoka kwa mwenye gari,” alisema.
Wakazi wa maeneo mengine nchini wataendelea kuzingatia kanuni zilizotangazwa na Wizara ya Afya iikiwemo marufuku ya kutotoka nje usiku lakini watakuwa huru kusafiri kaunti zingine isipokuwa Nairobi na viunga vyake, Kilifi, Kwale na Mombasa.
Rais Kenyatta alisema ni wazi ulimwengu uko vitani na serikali yake haitasita kuchukua hatua zaidi za kulinda Wakenya.
Alieleza kuwa serikali inatambua hatua hizo zitafanya maisha kuwa magumu zaidi na akaagiza Wizara ya Fedha kutumia Sh2 bilioni zilizotwaliwa kutoka kwa washukiwa wa ufisadi kusaidia familia maskini.
Mataifa mengi duniani yametangaza marufuku ya watu kutotoka baadhi ya maeneo na hata nje ya nyumba zao katika juhudi za kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.
Kufikia jana jioni watu wapatao milioni 1.3 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa kote duniani na zaidi ya elfu 70 kati yao kufariki.
Amerika iliendelea kuongoza kwa maambukizi idadi yake ikifika elfu 338 na vifo zaidi ya elfu tisa, ikifuatwa na Uhispania kwa maambukizi elfu 135 na vifo elfu 13. Italia ingali inaongoza kwa idadi ya juu ya walioaga dunia ikiwa na elfu 15.