Jengo la mkasa Eastleigh: nani alilala kazini?
KUPOROMOKA kwa jengo la orofa 18 katika Barabara ya 9, Eastleigh, Nairobi, kumeibua lawama kati ya taasisi zilizopaswa kusimamia ujenzi, huku kila upande ukikataa kuwajibika.
Gavana Johnson Sakaja alisema kaunti haikuidhinisha mipango ya jengo hilo na kwamba ujenzi ulisimamishwa mara mbili. Alidai baadhi ya vibali vilivyosambazwa mitandaoni vilikuwa bandia.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi Muchiri Nyaga alisema utoaji wa vibali na kusimamisha ujenzi ni jukumu la kaunti. Alisema tatizo la vibali haramu linapaswa kushughulikiwa ili kuzuia vifo.
“Polisi hawana uhusiano wowote na ujenzi wa majengo ya aina hiyo. Hayo ni majukumu ya serikali za kaunti pekee, na kwa hakika, kaunti zina idara za utekelezaji wa sheria ambazo zina mamlaka ya kusimamisha kabisa kazi yoyote ya ujenzi,” akasema Bw Muchiri.
Aliongeza kuwa madai ya gavana yanaonyesha mtu anayezama na kujaribu kushikilia chochote kile ili asizame.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Renson Ingonga alisema afisi yake haikuwa imepokea faili ya uchunguzi kutoka kaunti, na akaagiza Idara ya Upelelezi nchini (DCI) ichunguze iwapo maafisa wa kaunti, wajenzi au wataalamu walichangia mkasa huo.
Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025, huku kampuni ya 9th Street Plaza Limited ikitajwa kuwa ilihusika nao.
Mmiliki Mohamed Khatar Ali Noor alisema jengo lilikuwa na vibali vyote japo mhandisi Joseph Muturi Mugu alijitenga na mradi huo.
Mamlaka ya Kitaifa ya Utunzaji wa Mazingira (NEMA) ilikuwa imeiandikia kampuni hiyo Januari 2026 ikiitaka kuwasilisha michoro ya usanifu iliyo wazi kabla ya kushughulikia tathmini ya athari za mazingira.
Ripoti ya NCA ya 2015 ilionya kuwa majengo yanaweza kukaliwa bila ukaguzi wa mwisho na cheti cha kuruhusu matumizi. Ukaguzi wa 2018 ulipata majengo 723 kuwa hatari sana na 10,791 kutokuwa salama.
Mnamo 2024, Kamati ya Bunge la Kaunti ya Nairobi ilianzishwa kuchunguza madai ya vibali haramu, lakini ikavunjwa kabla ya kupokea barua muhimu.
Mwenyekiti wake Nasra Nanda alisema uchunguzi huo ulizimwa licha ya umuhimu wake.