Nani atafuata?
Na RICHARD MUNGUTI
WASIWASI umewakumba magavana wapatao sita baada ya mwenzao Mike Sonko wa Nairobi kufikisha idadi ya waliozimwa kuhudumu hadi watatu.
Uamuzi wa mahakama jana unamweka Bw Sonko kwenye kapu moja na Ferdinand Waititu wa Kiambu na Moses Lenolkulal Kasaine wa Samburu. Watatu hao watakaa kwenye baridi hadi kesi za ufisadi dhidi yao zisikizwe na kuamuliwa.
Kama ilivyokuwa imeagizwa kwa Bw Waititu na Bw Kasaine, Hakimu Mkuu Douglas Ogoti alimwagiza Bw Sonko asikanyange tena katika ofisi yake hadi kesi aliyoshtakiwa ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh381 milioni ikamilike.
Kati ya magavana ambao wamo kwenye hatari ya kufuata wenzao kwenye baridi ni wale ambao Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) inawachunguza na hata kuhoji baadhi yao.
Pia kuna wale ambao tayari wana kesi mahakamani. Hawa wana hofu kuwa huenda Mkurugenzi wa Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji akaomba mahakama itoe uamuzi wa wao pia kuondoka ofisini wakisubiri uamuzi wa kesi zao.
Walio na kesi ni Sospeter Ojamoong wa Busia anayekabiliwa na kesi ya ufisadi wa Sh8 milioni na Stephen Sang wa Nandi aliyeshtakiwa kwa kuongoza ung’oaji majani chai katika shamba la kibinafsi.
Okoth Obado wa Migori naye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya Sharon Atieno. Pia amekuwa akichunguzwa na EACC kwa madai ya wizi wa Sh2 bilioni
Wengine ambao wanamulikwa na EACC ni Alex Tolgos wa Elgeyo Marakwet kuhusu madai ya ufujaji wa Sh200 milioni za umma.
Gavana Mwangi wa Iria wa Murang’a naye amekuwa akiandamwa na maafisa wa EACC kuhusu Sh390 milioni za ununuzi wa shamba la ekari 30 huku Ali Korane wa Garissa akifuatwa kuhusu Sh48 milioni zinazohusu utoaji tenda.
Hakimu Ogoti alisema Kifungu nambari 10 kinachowataka maafisa wa umma kuletea afisi wanazohudumu heshima lazima kizingatiwe katika suala la Bw Sonko.
Mawakili Steve Mogaka na Dunstan Omari wanaotetea Kaunti ya Nairobi, walizimwa na hakimu waliposema kuwa Kaunti ya Nairobi haina Naibu wa Gavana kufuatia kujiuzulu kwa Polycap Igathe.
“Kutakuwa na mgogoro wa kikatiba katika Kaunti ya Nairobi iwapo Sonko ataagizwa akome kutekeleza majukumu yake,” Bw Mogaka alimweleza hakimu.
Lakini Bw Ogoti alisema anajua suala la naibu wa gavana wa kaunti hii ya Nairobi limekuwa likijadiliwa katika hafla mbalimbali lakini sheria lazima ifuatwe.
Awali, wakili George Kithi anayemwakilisha Bw Sonko aliomba gavana huyu aruhusiwe kuendeleaa kuhudumu kwa vile hana naibu na aking’atuliwa kutakuwa na mtafaruku katika utendakazi Nairobi.
Akimwachilia Sonko kwa dhamana ya Sh15 milioni pesa taslimu ama bodi ya Sh30 milioni, Bw Ogoti alimruhusu gavana huyo pamoja na wafanyakazi wa kaunti walioshtakiwa pamoja naye kurudi afisini wakiandamana na maafisa wa polisi kuchukua mali zao za kibinafsi.
Bw Sonko na washtakiwa wenzake waliagizwa wasiwavuruge mashahidi kwa kuwatisha ama kuwapa vishawishi wasifike kortini kutoa ushahidi dhidi yao.
Pia, wahusika wote katika kesi hiyo walitakiwa wasiijadili katika mitandao ya kijamii.
Bw Sonko na wenzake wamekanusha mashtaka ya ubadhirifu wa Sh381 milioni.
Kesi itatajwa tena Januari 15, 2020.