Habari

Nassir aonya ‘wanafiki’ katika chama cha ODM

Na MISHI GONGO November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ametoa ilani kwa wanachama wa ODM anaowataja kuwa ‘wanafiki’ kuwa wataanikwa hivi karibuni.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara Kilifi Novemba 16, 2025, Bw Nassir, ambaye pia ni mmoja wa manaibu viongozi wa ODM, alisema ukweli kuhusu misukosuko chamani utabainika karibuni.

“Kuna wengine ndani ya chama ambao ni wanafiki. Wanapokea hela kujaribu kufanya chama kipasuke lakini watafeli,” akasema.

Bw Nassir alisema ODM imepitia mengi kwa miezi 20 iliyopita lakini chama kiko imara.

“Mti mkubwa ukianguka wana ndege huyumba. Wapo wanaotaka tukivunje chama lakini hawatafanikiwa,” akasema Bw Nassir.

Wakati huo huo, aliahidi ushindi katika chaguzi ndogo zinazotarajiwa wiki ijayo, akimpigia debe mgombea wa chama cha ODM wa Kilifi Magharibi, Bw Harrison Kombe.

Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alionya viongozi wanaopania kururusha wenzao kutoka chamani.

“Hatuwezi kuunda serikali bila umoja. Acheni kusukumana nje. 2027 tunahitaji idadi na mikakati,” akasema.

Gavana wa Kisii, Bw Simba Arati, ambaye pia ni naibu kiongozi, aliwatuliza wanachama akisema kuwa roho ya mwenda zake Raila bado ipamoja nao.

Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohammed, alikosoa misimamo mikali ya Katibu Mkuu Edwin Sifuna akisema hataondoa Pwani katika ODM.