Habari

Mwalimu atupwa ndani kwa kujeruhi mwanafunzi nyeti

May 28th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na STEPHEN NJUGUNA

POLISI katika Kaunti ya Nyandarua, wamemkamata mmoja wa walimu watatu ambao Alhamisi iliyopita walidaiwa kumpiga mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Kamukunji na kumjeruhi sehemu za siri.

Kulingana na mkuu wa polisi eneo la Ol-Jooro Orok (OCPD), Bw Sylvester Githungo, mwalimu huyo alikamatwa Jumamosi jioni akiwa nyumbani kwake Ol Jooro Orok.

“Tunamzuilia mshukiwa kuhusiana na kushambuliwa kwa mwanafunzi huyo. Hata hivyo, wenzake wawili hawajapatikana,” alisema Bw Githungo.
Alisema maafisa wa polisi na wa upelelezi wamepata habari wanazotumia kuwasaka walimu hao wawili.

“Tunaendelea kuchunguza kesi hii na ninataka kuomba umma kutulia. Ninataka kuwahakikishia kwamba washukiwa wote watakamatwa,” alisema. Afisa huyo aliongeza kwamba mshukiwa aliyekamatwa atafikishwa kortini leo.

Madaktari katika hospitali kuu ya Kaunti ya Nyahururu wanasema kwamba mvulana huyo anaendelea kupata nafuu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu zake za siri.

“Alifanyiwa upasuaji uliofaulu kurekebisha sehemu zake za siri na sasa yuko katika hali nzuri. Anaweza kutembea pole pole, kupitisha mkojo na kujipatia chakula,” daktari mmoja katika hospitali hiyo alisema.

Mnamo Ijumaa, kamishna wa Kaunti ya Nyandarua Boaz Cherutich aliagiza polisi kuchunguza kisa hicho baada ya umma kutaka walimu hao wakamatwe.

Kabla ya Bw Cherutich kutoa hakikisho hilo, maafisa wa elimu eneo hilo walikuwa wamelaumu vyombo vya habari kwa kuharibu sifa za shule hiyo na kuchochea chuki kati ya walimu na wazazi.

Akihojiwa baada ya mvulana huyo kujeruhiwa, mamake alisema alipokea simu kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule akimfahamisha mwanawe alikuwa na shida shuleni.

Alisema alipofika shuleni alimpata mwanawe akiwa amepoteza fahamu na baadhi ya walimu wakijaribu kumpa huduma ya kwanza.

Bi Wangeci alisema kaptula ya mvulana huyo ilikuwa na damu na alipouliza walimu kilichotendeka hakuna aliyemjibu. Baadaye alifahamishwa na wanafunzi kwamba mwanawe alijeruhiwa na walimu wakimwadhibu walipompata akicheza darasani. Mwanamke huyo alisema anataka haki itendeke.