HabariSiasa

Ndindi Nyoro mwiba kwa Uhuru

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NYAMBEGA GISESA

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro, ambaye alikuwa mtetezi sugu wa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017 hatimaye amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa rais, japo chini kwa chini.

Kutokana na uhasama huo, Rais amelazimika kuondoka mkutanoni mara mbili mbunge huyo anapoanza kuhutubu.

Mahakama Kuu ilipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais, Bw Nyoro alitishia kujiuzulu endapo Rais Kenyatta angebwagwa na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa marudio uliofanyika Oktoba 26, 2017. Lakini sasa, mbunge huyo chipukizi amegeuka kuwa mwiba wa kisiasa kwa Rais Kenyatta.

Kama ishara ya kukerwa na mbunge huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa vuguvugu la Tanga Tanga linalounga mkono Naibu wa Rais William Ruto, Rais Kenyatta kwa mara nyingine, mwezi uliopita, aliondoka nje ya hema, Bw Nyoro aliposimama kuhutubia waombolezaji.

Rais Kenyatta alirejea baada ya Bw Nyoro kumaliza kuhutubia waombolezaji waliohudhuria mazishi ya aliyekuwa mfanyabiashara mashuhuri Thayu Kamau Kabugi. Rais aliposimama kuhutubia waombolezaji, alimshambulia Bw Nyoro kwa kutangatanga nchini akipiga domo la kisiasa.

Mwaka jana, Rais Kenyatta pia aliondoka nje Bw Nyoro alipokuwa akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya mwanasiasa mkongwe Kenneth Matiba.

Bw Nyoro si mwiba tu kwa Rais Kenyatta bali kwa Bw Odinga pia.

Wiki chache zilizopita, Bw Odinga alimrejelea Bw Nyoro kama ‘kichaa’ baada ya kuwasilisha mswada bungeni unaolenga kupunguza mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Wanasiasa wa Tanga Tanga wamekuwa wakidai kwamba DCI na DPP wanatumiwa kisiasa kupitia vita dhidi ya ufisadi kusambaratisha azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022. Matamshi ambayo Bw Nyoro amekuwa akitoa dhidi ya Bw Odinga yamemfanya kuchukiwa na wafuasi wa kiongozi wa ODM.

Wakati wa mechi ya Gor Mahia iliyochezwa uwanjani Kasarani wiki iliyopita, mbunge huyo alilazimika kuondoka upesi kabla ya mechi kuisha ili kukwepa ghadhabu za mashabiki wa timu hiyo ambao wengi wao ni wafuasi wa Bw Odinga.

Huku Rais Kenyatta na Bw Odinga wakionekana kukerwa na mbunge huyo chipukizi, Naibu wa Rais Dkt Ruto anamuona kama shujaa na nguzo muhimu katika kampeni zake za 2022.

“Nimetembea kote nchini na bila shaka mbunge wenu (Nyoro) ni miongoni mwa viongozi wachache wapenda maendeleo nchini,” akasema Dkt Ruto mazishini.