'Ndoa ya UhuRuto ilivunjika kitambo'
Na WAANDISHI WETU
WABUNGE wa Jubilee wanaopinga azma ya Naibu Rais William Ruto ya kugombea urais 2022, sasa wanadai alivunja uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta kwa kutaka kupimana nguvu naye.
Wabunge hao walifichua kuwa, Rais Kenyatta ataungana na wanasiasa wanaounga sera zake kubuni muungano utakaounda serikali ijayo.
“Ni sharti ieleweke kwamba Naibu Rais alimuacha Rais kitambo na akaanza kumpinga. Anawafadhili wabunge wanaohudumu mara ya kwanza bungeni kupigia debe azma yake ya urais 2022 na kumharibia Uhuru,” alisema mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda.
Bw Kamanda alisema mipango inaendelea kati ya rais na viongozi wa vyama vya ODM, Wiper, ANC na KANU ya kuwa na muungano mkubwa wa kuunganisha Wakenya.
Wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Joshua Kutuny (Cherangany) Peter Mwathi (Limuru) na Robert Mbui wa Kathiani waliunga kauli ya Bw Kamanda.
Kundi la ‘Kieleweke’ analoongoza Bw Kamanda, limeanza kupigia debe muungano huo utakaoshirikisha vigogo watatu wa upinzani pamoja na Rais Uhuru ili kumenyana na Naibu Rais Ruto, katika Uchaguzi Mkuu 2022.
Wadhifa tofauti
Pia limedokeza kuwa linaunga mkono mabadiliko ya kikatiba ili kumwezesha Rais Kenyatta kuendelea kuhudumu baada ya 2022 japo katika wadhifa tofauti, Katiba ikibadilishwa.
Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Dagoreti Kaskazini Dennis Waweru, wanaodhani Rais Kenyatta atastaafu watashangaa sana.
Aliyekuwa mbunge Mukurweini Kabando wa Kabando amepuuzilia mbali umaarufu wa kundi la ‘Tangatanga’ linalomuunga Dkt Ruto akisema muungano mpya unaotarajiwa kubuniwa hauwezi kutishwa au kushindwa kwa vyovyote na kwamba mabadiliko ya Katiba yanayosubiriwa ndiyo yatakayoamua hatima ya taifa.
“Sio kuhusu 2022 lakini ni kuhusu kizazi kijacho. Kikosi cha ‘Tangatanga’ kinatikisa Mlima Kenya lakini punde ujasiri wa ‘Tangatanga’ utatokomea mbali. Wanacheza kabla ya ngoma kupigwa. BBI itaangaza mwanga utakaokuwa vigumu kukataa,” alisema Kabando.
Kulingana na Bw Kabando, Dkt Ruto amekuwa akiwafadhili wabunge kupigia debe azma yake ya urais 2022 na kueneza madai kwamba familia za Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Jaramogi Oginga Odinga zinataka kuendeleza tawala za kifamilia.
“Rais ni sharti awe imara kwa sababu kuna propaganda nyingi lakini tuko tayari kukabiliana nazo. Ni sharti Rais asimame kuwatafuta marafiki wake,” akashauri Kabando.