Habari

Ni gavana spesheli?

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WAKATI magavana wanaoshtakiwa kwa ufisadi wanajipata kwenye baridi kwa kuzuiwa kutekeleza majukumu yao baada ya kupigwa marufuku kukanyaga ofisi zao na mahakama au hata kuondolewa mamlakani, kwa Gavana Mike Sonko wa Nairobi, mambo ni tofauti.

Kwake, kuzuiwa kukanyaga ofisi yake rasmi katika City Hall hakujamzuia kutekeleza majukumu yake. Jambo hili linaibua maswali kama yeye ni spesheli kuliko magavana wengine wanne.

Japo anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi kama wenzake hao, Bw Sonko anaendelea kuchapa kazi kutoka ofisi yake ya kibinafsi katika eneo la Uppehill, kukutana na Rais, kualikwa kuhudhuria hafla Ikulu na nyingine za rais na hata kuruhusiwa kuhutubu.

Hii, pamoja na kuruhusiwa kuhudhuria hafla za rais, kunamfanya kuonekana spesheli na tofauti na wenzake ambao wamezuiwa kuhudumu kutoka ofisi zao za kibinafsi au kutekeleza hafla zozote rasmi hadi kesi zao zitakapoamuliwa.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinard Waititu anayekabiliwa na kesi ya ufisadi inayohusisha uporaji wa Sh537 milioni alizuiwa kuhudumu kutoka ofisi ya kibinafsi na kisha akaondolewa ofisini. Kabla ya madiwani kumuondoa ofisini, alizuiwa kuketi eneo lililotengewa magavana wakati wa sherehe za kitaifa.

Mwaka 2019 Bw Waititu alitimuliwa jukwaa la watu mashuhuri wakati wa sherehe za Mashujaa Dei mjini Mombasa.

Mwaka huu 2020, Bw Sonko alialikwa katika sherehe za Madaraka katika Ikulu. Vile vile, Bw Sonko amekuwa akihudhuria hafla za kitaifa bila kuzuiwa, kualikwa Ikulu kwa sherehe tofauti na kujumuika na Rais katika hafla jijini anakoruhusiwa kuhutubu.

Rais Kenyatta pia amemhimiza kushirikiana na Idara ya Huduma la jiji la Nairobi (NMS) kufanya kazi licha ya kusisitiza kwamba maafisa wanaoshtakiwa kwa ufisadi wanafaa kuondoka ofisini.

“Sitaki kusikia vita vya kisiasa Nairobi. Ndugu zangu (Sonko na Mkurugenzi wa NMS, Mohammed Badi) fanyeni kazi pamoja. Si kila saa ni vita na matusi. Jukumu letu ni kuhudumia wananchi,” alisema Rais alipotoa hati za kumiliki ardhi kwa wakazi wa Embakasi Agosti 12, 2020.

Madiwani wa bunge la kaunti ya Nairobi walipopanga kumuondoa ofisini, Rais Kenyatta alimuokoa kwa kuwaita katika mkutano Ikulu kuwashawishi wasimtimue.

Hii ni tofauti na yaliyompata Bw Waititu. Mchakato wa kumuondoa ofisini Gavana wa Migori Okoth Obado pia umeanza wiki moja baada ya kukanusha mashtaka ya ufisadi. Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal aliyeshtakiwa kwa ufisadi kabla ya Bw Sonko angali katika baridi ya kisiasa baada ya kupigwa breki kuhudumu.

Wenzake walioshtakiwa kwa madai ya ufisadi wanaponyamaza kusubiri kesi zao ziamuliwe, Bw Sonko anaendelea na shughuli zake kama kawaida kutoka ofisi yake ya kifahari ya kibinafsi, kukutana na wakazi wa Nairobi, kuhutubia wanahabari, na kukagua miradi ya maendeleo.

Katika uamuzi aliotoa mwaka jana, Jaji Mumbi Ngugi alisema kuwa Magavana wanaoshtakiwa kwa ufisadi wanafaa kuondoka ofisini kama maafisa wengine wa serikali na manaibu wao kutekeleza majukumu yao.

Bw Sonko amejivuta kumteua naibu tangu Polycape Igathe alipojiuzulu Januari 2018. Wadadisi wanasema kwamba, kumuondoa ofisini kunaweza kusababisha mzozo wa uongozi na uchaguzi mdogo ambao serikali inahisi haufai wakati huu viongozi wakuu wamegawanyika.