Ni rasmi kwamba riba za benki zitakuwa juu sasa
Na CHARLES WASONGA
NI rasmi sasa kwamba mikopo ya benki itakuwa ghali mno kwani benki zitakuwa huru kutoza viwango vya riba zinavyotaka.
Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini Mswada wa Fedha wa 2019 kuwa sheria.
Miongoni mwa sheria zingine, sheria hiyo imeifanyia mageuzi sehemu ya 33b ya Sheria za Benki na ambayo inadhibiti viwango vya riba vinavyotozwa na benki kwa mikopo zinazotoa kwa wateja wao.
Kipengee hicho kiliondolewa Jumanne baada ya wabunge kushindwa kutupilia mbali memoranda ya Rais iliyopendekeza kuondolewa kwa sheria ya udhibiti wa riba iliyopitishwa mnamo Septemba 2016.
Hii ni baada ya wabunge wengine kususia kikao cha bunge wakati suala hilo lilifaa kuamuliwa kupitia upigaji kura.
Angalau wabunge 233 (yaani thuluthi mbili ya wabunge wote 349) walihitajika kupinga pendekezo hilo la Rais.
Hata hivyo, ni wabunge 161 pekee waliokuwepo ukumbini Jumanne alasiri; hali iliyomfanya Spika Justin Muturi kusitisha upigaji kura kuamua hatima ya pendekezo la Rais.
Na kwa sababu hiyo, pendekezo la Rais lilijumuishwa moja kwa moja katika mswada huo ambao ameutia saini Alhamisi, Novemba 7, 2019.
Rais Kenyatta alisema kuondolewa kwa sheria ya kudhibiti riba kunalenga kuwezesha wafanyabiashara wadogowadogo kupata mikopo kutoka benki ili kupanua biashara zao.
“Hatua hii pia inawazima walaghai ambao wamekuwa wakitoa mikopo kwa wafanyabiashara kwa riba ya juu na hivyo kuwapunja,” akasema Rais Kenyatta katika memoranda yake aliyowasilisha bungeni majuma mawili yaliyopita.
Waliohudhuria hafla fupi ya kutiwa saini kwa mswada huo katika Ikulu ya Nairobi walikuwa ni; Spika wa Muturi, Mwanasheria Mkuu Paul Kihara, kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yatani miongoni mwa maafisa wengine wa serikali.