HabariSiasa

Niko tayari kuungana na UhuRaila kuunganisha Wakenya – Kalonzo

May 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FRANCIS MUREITHI

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema yuko tayari kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi za kuunganisha Wakenya na kuzika siasa za mgawanyiko.

Bw Musyoka alipongeza hatua ya Rais Kenyatta kuanza mikakati ya kuunganisha Wakenya kwa ushirikiano na kinara wa NASA Raila Odinga mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Musyoka pia alimpongeza rais kwa kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kugawanya Wakenya wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017.

Makamu huyo wa rais wa zamani, alisema hayo alipokuwa akihutubia wanahabari katika hoteli moja eneo la Elementaita, Nakuru wakati wa kufunga kongamano la siku mbili la viongozi wa Wiper.

“Ningependa kumpongeza Rais Kenyatta kwa kujitokeza wazi na kuomba Wakenya msamaha. Ni viongozi wachache mno wanaoweza kunyenyekea na kuomba wananchi msamaha. Nimempa hongera kwa hilo. Huu ni wakati wa kusamehe na kuhubiri amani,” akasema Bw Musyoka.

 

Kukutana na Mzee Moi

Bw Musyoka alisema anapanga kukutana na Rais Mstaafu Daniel arap Moi hivi karibuni.

“Ninapanga pia kumtembelea Rais Mstaafu Mwai Kibaki na mama yake rais, Mama Ngina Kenyatta,” akasema Bw Musyoka.

Bw Musyoka alimkejeli Naibu wa Rais William Ruto ambaye juhudi zake za kukutana na Mzee Moi ziligonga mwamba wiki iliyopita.

“Walioshindwa kumwona Rais Mstaafu Moi wajaribu tena,” akasema Bw Musyoka huku akisababisha kicheko.

Alisema mwafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga unastahili kuleta maendeleo na wala si kusuluhisha mizozo ya kisiasa tu.

Alisisitiza kuwa muungano wa NASA bado ni thabiti huku akisema kuwa atashinikiza NASA isajiliwe kama chama cha kisiasa. Alisema Bw Odinga hajajiunga na chama cha Jubilee na bado yuko katika Upinzani.

Alisema kabla ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kusalimiana, yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kushinikiza viongozi hao wawili wakutane ili kuzungumza.

“Nilikuwa katika mstari wa mbele kuwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga wakutane na kusitisha siasa za mgawanyiko. Inaonekana Bw Odinga alisikia wito wangu na akakubali kukutana na Rais Kenyatta japo hakunifahamisha,” akasema Bw Musyoka.

“Chama cha Wiper kiko tayari kuanzisha mchakato wa kuunganisha nchi na kuhubiri amani,” aliongeza.

Bw Musyoka pia alisema anaunga mkono Katiba kufanyiwa mabadiliko.

“Niliitwa tikitimaji kwa sababu nilisema kuwa Katiba ilifaa kuangaliwa kwa makini. Sasa Wakenya wameona umuhimu wa niliyosema.

Chama cha Wiper kinaunga mkono mabadiliko ya Katiba na tunafaa kujadili suala hili kwa makini,” alisema Musyoka.