Nimefika mwisho!
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amemnyooshea kidole cha lawama naibu wake William Ruto kama kikwazo chake katika kutimiza ahadi alizowapatia Wakenya.
Ingawa hakumtaja Dkt Ruto moja kwa moja, Rais Kenyatta kwenye mahojiano na gazeti la Daily Nation alionyesha kuvunjika moyo na naibu wake kwa kukosa kuunga mkono utekelezaji wa ajenda zake, na badala yake kuanza kampeni za mapema za kumrithi 2022.
“2019 yote nilikuwa nikiwasihi watu: ‘Tafadhalini acheni tuangazie Ajenda Nne Kuu kwanza, kwani wakati wa siasa bado’… Siwezi kuendelea kubembeleza watu. Sina muda!” akasema Rais Kenyatta.
Mwaka 2019 Rais alieleza kukasirishwa na kundi la ‘Tangatanga’ linalojumuisha wanaounga azma ya Dkt Ruto kuwania urais 2022, kwa kutumia muda mwingi kwenye ziara maeneo mengi ya nchi wakimpigia debe.
“Usikubali matarajio ya kesho yakuzuie kufanya mambo ya leo kwa sababu unachofanya leo ndicho kitaamua utakapokuwa kesho,” akasema Rais akionekana kumlenga Dkt Ruto kwa kuanza mapema siasa za kumrithi.
Kwenye mahojiano hayo, Rais Kenyatta alionekana kumlimbikizia lawama Naibu Rais kuhusu kufifia kwa kasi ya utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu na vita dhidi ya ufisadi.
“Iwapo hutaki kuunga mkono miradi, ni sawa! Unaweza kwenda kufanya mambo mengine,” akasema Rais Kenyatta.
“Ikiwa unahisi huwezi kufanya kazi kufanikisha ajenda zangu, mbona usiondoke na uniache niweke mtu ambaye yuko makini katika kunisaidia kutimiza ahadi nilizowapa Wakenya 2017 na 2013? Kama unahisi hujatosheka, uko huru kufanya mambo mengine yote unayotaka,” akaeleza.
“Ninataka kufanya kazi na watu ambao hawapingi ajenda zangu kwa Wakenya. Ninataka watu ambao wataunga mkono ajenda hizo. Katika demokrasia, iwapo hufurahishwi na jinsi kiongozi anavyoelekea, basi! Hakuna lingine,” akaeleza Rais.
Akaongeza: “Kuna mambo ambayo niliwaahidi Wakenya uwanjani Kasarani nilipoapishwa. Niliahidi nitatimiza Ajenda Nne Kuu na bado niko kwenye mkondo huo. Pia nilisema nitamaliza ufisadi nchini.”
Ajenda Nne Kuu alizotangaza Rais alipoapishwa kwa muhula wa pili mnamo 2017 ni makazi, viwanda, afya na chakula. Lakini kufikia sasa hakuna hatua kubwa zilizopigwa huku ikibaki miaka miwili pekee Rais Kenyatta kung’atuka madarakani.
Msukumo wa vita vya ufisadi pia umefifia.
Kulingana na mahojiano na Daily Nation, Rais Kenyatta alionyesha mtazamo kuwa naibu wake alizingatia zaidi azma yake ya kisiasa badala ya kuunga mkono ajenda ya bosi wake.
Rais alionyesha dalili za mwanzo za kupoteza imani na Dkt Ruto mwaka 2019 alipomwondoa kama msimamizi mkuu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukabidhi wajibu huo kwa Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i.
Kwa miezi kadhaa sasa Dkt Ruto pia hajakuwa akihudhuria hafla katika Ikulu wala mikutano ya Baraza la Kitaifa la Usalama ambapo ni mwanachama.
Wakati Rais Kenyatta alipotangaza vita dhidi ya ufisadi, Dkt Ruto alikosoa jinsi mchakato huo ulivyokuwa ukiendeshwa akisema ulionekana kulenga wandani wake kisiasa.
Dkt Ruto pia amekwaruzana na bosi wake kwa kupinga Mpango wa Maridhiano (BBBI) na handisheki kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, akidai waziri huyo mkuu wa zamani ana nia ya kuvunja Jubilee na kuingia serikalini kwa njia za mkato.
“Nasikita kuwa ninapojaribu kuunganisha Kenya, baadhi ya watu wanaona kama ninawatenga. Simpigi vita mtu yeyote. Ninawafanyia kazi Wakenya wote milioni 47,” akasema Rais Kenyatta.
Katika mchakato unaoendeshwa na Rais dhidi ya Dkt Ruto, wandani wake wameanza kuondolewa kwenye nyadhifa za Seneti na Bunge la Kitaifa.
Katika Seneti wandani wa Naibu Rais waliolishwa sakafu ni Kipchumba Murkomen (Kiongozi wa Wengi), Kithure Kindiki (Naibu Spika) na Susan Kihika (Kiranja wa Wengi) kati ya wengine walioondolewa kwenye kamati za Seneti.
Wiki ijayo inatarajiwa kuwa zamu ya kuwaondoa wafuasi wa Dkt Ruto katika Bunge la Kitaifa. Kati ya wanaolengwa ni Aden Duale (Kiongozi wa Wengi), Ben Washiali (Kiranja wa Wengi) na Kimani Ichung’wah (Kamati ya Bajeti).