Habari

Nimemjenga Uhuru – Ruto

January 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto amedai kwamba ndiye aliyemjenga Uhuru Kenyatta kisiasa hadi akafanikiwa kuwa Rais.

Dkt Ruto alisema alimfahamu Bw Kenyatta mnamo 1998 alipotumwa na Rais Mstaafu Daniel Moi kumrai Bw Mark Too kujiuzulu kama mbunge wa kuteuliwa ili kumpa nafasi Bw Kenyatta.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV Alhamisi usiku, Dkt Ruto alisema kuwa, ndiye mwanasiasa pekee aliyejitolea zaidi ili kumjenga Rais Kenyatta kisiasa hadi pale alipofika.

Alisema haikuwa rahisi kumshawishi Bw Too kujiuzulu.

“Ikiwa kuna mwanasiasa aliyejitolea sana kwa manufaa ya Rais Kenyatta, basi ni mimi. Nimesimama naye hata katika nyakati ngumu zaidi. Kwa mfano, haikuwa rahisi kwangu kumrai Bw Too kujiuzulu kama Mbunge Maalum ili kumpa nafasi Bw Kenyatta,” akasema Dkt Ruto.

Alisema mnamo 2002 baada ya Bw Moi kumtangaza Uhuru kuwa mwaniaji urais wa chama cha Kanu, alimuunga mkono licha ya baadhi ya wanasiasa kuondoka na kubuni chama cha Liberal Democratic Movement (LDP).

Baadhi ya wanasiasa walioondoka Kanu kulalamikia hatua ya Bw Moi ni kinara wa ODM Raila Odinga, Prof George Saitoti, William Ole Ntimama, Joseph Kamotho kati ya wengine.

Hata hivyo, Dkt Ruto alisema alimuunga mkono Rais Kenyatta na hata kumfanyia kampeni hadi pale walikubali kushindwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliyegombea kwa tiketi ya muungano wa NARC kwenye uchaguzi mkuu wa 2002.

“Tulipoondoka kwenda kuwahutubia wanahabari kukubali kushindwa, tulikuwa zaidi ya watu 60. Hata hivyo, tulipofika kuhutubu, tulikuwa watu watatu pekee; mimi, Rais Kenyatta na mtu mwingine mmoja,” akasema Dkt Ruto.

Kwa mujibu wa Dkt Ruto, mwaka 2012 ndipo walikumbwa na wakati mgumu zaidi, baada ya aliyekuwa Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Moreno Ocampo kuwataja kuwa miongoni mwa watu sita waliohusika kwenye ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008 ambapo watu zaidi ya 1,000 walipoteza maisha yao.

“Hata baada ya masaibu yaliyotukumba katika ICC, niliendelea kumuunga mkono bila sharti lolote,” akasema.

Alieleza kuwa imani yake kwa uwezo wa Rais Kenyatta ndiyo ilimfanya kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017, bali si kwa tumaini kwamba, Rais angerudisha mkono kwa kumuunga kuwa mrithi wake.

Kauli yake inajiri huku siasa za urithi wa Rais Kenyatta mnamo 2022 zikizidi kushika kasi, ambapo ameonekana kutengwa, hasa baada ya Rais kumkumbatia kinara huyo wa upinzani.

Dkt Ruto amekuwa akikosolewa na baadhi ya wandani wa karibu wa Rais Kenyatta kwa kuwa kikwazo kikuu kwa utendakazi wake, kwa kuendesha kampeni za mapema za 2022. Hata hivyo, alitaja hali hiyo kuwa ya kawaida, ambayo hutokea kila wakati siasa za urithi zinapokaribia, akirejelea urithi wa Mzee Jomo Kenyatta na Bw Kibaki mnamo 1978 na 2012 mtawalia.

Dkt Ruto alisema kuwa hataondoka katika Chama cha Jubilee (JP) hata baada ya uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika mnamo Machi akisema anaamini katika maono, ajenda na malengo yake.