Habari

Nitampigania Ruto hadi kifo, asema Kiunjuri

February 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GAKUU MATHENGE

ALIYEKUWA Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri amekariri kuwa hatakoma kuunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu mwaka wa 2022 hata akitishwa.

Huku akijiita jenerali wa Dkt Ruto, Bw Kiunjuri alisema yuko tayari kusimama na Naibu Rais hata akikosa kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu ujao na kuingia upinzani.

“Nitaendelea kuwa jenerali mkuu wa Naibu Rais hadi mwisho, akiunda serikali na hata kama hataunda serikali,” Bw Kiunjuri alisema kwenye mahojiano na ‘Taifa Jumapili’.

“Hata kama tutakufa, roho zetu zitaendelea kuzungumza kaburini,” aliongeza.

Bw Kiunjuri alisema kuwa ameamua kuunda chama kipya cha kisiasa, The Service Party (TSP) ili kufufua nyota yake ya kisiasa baada ya kufutwa kazi “bila sababu”.

Chama cha Government of National Unity (GNU) ambacho Kiunjuri aliongoza ni mojawapo ya vyama 12 vilivyounganishwa ili kuundwa kwa chama cha Jubilee.

“Inasikitisha kuwa nilifutwa kazi ya uwaziri katika serikali ya Jubilee bila sababu ilhali mimi ni mshika dau mkuu ndani ya serikali. Mimi sikuwa mwanachama wa kawaida katika Jubilee kurushwa nje kiholela,” Bw Kiunjuri.

Wanasiasa wengine ambao walikuwa viongozi wa vyama vya kisiasa kabla ya kuteuliwa mawaziri ni; Eugene Wamalwa (Waziri wa Ugatuzi) na Najib Balala (Utalii).

“Tulishawishiwa kuvunja vyama vyetu na hati ya makubaliano ikahifadhiwa katika afisi ya msajili wa vyama mnamo 2016. Kulingana na hati hiyo, vyama tanzu havikuruhusiwa kudhamini wagombeaji,” alisema Bw Kiunjuri.

Itakumbukwa kwamba ni Rais Uhuru Kenyatta aliyemshawishi Bw Kiunjuri ajiondoe kutoka kinyang’anyiro cha ugavana wa Laikipia 2017. Alimwambia ajiunge na kundi la kampeni ya urais akisubiri kuteuliwa katika baraza la mawaziri.

Na Rais Kenyatta alipounda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Kiunjuri aliteuliwa kuwa Waziri wa Ugatuzi kabla ya kuhamishwa hadi wizara ya Kilimo mnamo 2018.

“Nilikuwa na nafasi nzuri ya kushinda kiti cha ugavana wa Laikipia katika uchaguzi mkuu wa 2017,” akasema.

Alipoulizwa ikiwa chama kipya alichokibuni kitavuruga umoja wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya, Bw Kiunjuri alisema raia ni werevu na wana uwezo wa kutofautisha kati ya wale ambao wanahimiza umoja “halali” na wale ambao wahimiza umoja kupitia vitisho.

Kuhusu mpango wa maridhiano (BBI), Bw Kiunjuri alisema suala hilo halipasi kutumiwa kuleta mgawanyiko miongoni mwa wakazi wa Mlima Kenya.

“Umoja wa watu wetu ni muhimu zaidi. Huu mpango wa BBI usitumiwe kuleta mgawanyiko haswa kuhusu mfumo bora wa utekelezaji wa mpango huo,” akasema.

Bw Kiunjuri alisema ataendelea kusimama na Dkt Ruto licha ya kutishwa na watu ambao hakutaja majina.