Njama ya Uhuru, Raila kusukuma BBI
Na JUSTUS OCHIENG
RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, wanapanga kushawishi magavana kupigia debe ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).
Hayo yamefichuka huku joto likizidi kupanda kuhusu ripoti hiyo ambayo haijatolewa rasmi.
Viongozi hao wawili wanataka kunufaika kutokana na ushawishi wa magavana pamoja na uwezo wao wa kifedha kufikia wananchi wengi zaidi kitaifa na kupigia chapuo mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Imesemekana Rais Kenyatta na Bw Odinga wana wasiwasi kuhusu jinsi ambavyo mgawanyiko umetokea kabla ripoti kutolewa na hivyo basi magavana wanatarajiwa kushawishi wananchi kwamba ni ripoti muhimu kwao.
Hii ni licha ya kuwa magavana pia wana mchakato wao wa marekebisho ya katiba ambao ni Ugatuzi Initiative kwa lengo la kuimarisha serikali za kaunti.
Kuunganisha mapendekezo
Duru zinasema Rais na Bw Odinga wanawazia pia kuunganisha mapendekezo ya BBI na yale ya Ugatuzi Initiative ili kuzuia kuwahangaisha wananchi na mapendekezo mengi ya kurekebisha katiba.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Bw Wycliffe Oparanya jana alisema mchakato wao ungali unasonga mbele.
Alisema tayari wamewasiliana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili wapewe mwelekeo.
Gavana huyo wa Kakamega alisema wanatazamia pia kuchanganua BBI ili kuona kama kuna uwezekano wa kuunganisha ripoti hiyo na Ugatuzi Initiative hasa kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti.
“IEBC ilitushauri kusubiri hadi uchaguzi mdogo wa Kibra ukamilike kabla watushauri kuhusu hatua tunayofaa kufuata. Tunajihadhari pia ili tusiwe na mapendekezo yanayofanana na yale ya BBI,” akasema. Aliongeza: “Ikibainika kwamba mapendekezo ya BBI yanafanana na yetu hasa kuhusu kuongeza fedha za ugatuzi, basi kuna uwezekano mkubwa tutaungana. Hakutakuwa na haja ya ushindani.”
Katika eneo la Nyanza, Gavana wa Kisumu Anyang’ Nyong’o aliambia viongozi wasubiri ripoti kamili ya BBI badala ya kueneza uvumi kuhusu mapendekezo yaliyomo. Lakini Gavana wa Siaya Cornel Rasanga alisema wazi kwamba ataunga mkono BBI kikamilifu.
Magavana wanne kutoka Mlima Kenya walimwomba Rais Kenyatta afanye mipango haraka kutoa ripoti ya BBI ili kupunguza taharuki inayoenea nchini, alipozungumza Nairobi mnamo Jumanne.
Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru alikashifu wapinzani wa BBI wanaotoka Mlima Kenya akisema msimamo wao ni sawa na kumkosea heshima Rais Kenyatta.
Duru zilisema Rais Kenyatta na Odinga pia watatumia maseneta, wabunge na madiwani kupigia debe BBI ili iungwe mkono na mabunge mengi ipasavyo ya kaunti endapo kutakuwa na pendekezo la kurekebisha katiba.