Njoroge Gavana Bora wa benki katika mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara
Na CHARLES WASONGA na MAGDALENE WANJA
GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Patrick Njoroge ametawazwa kama Gavana Bora wa benki katika mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, wakati wa tuzo ya mwaka huu ya watungaji sera bora, maarufu kama ‘2019 Global Markets Award’.
Bw Njoroge alitambuliwa na jarida la GlobalMarkets .
Amepokea tuzo hiyo kwa kufanya mabadiliko katika sekta ya benki nchini na upanuzi wa domestic capital markets.
“Bw Njoroge ameiongoza sekta ya benki katika hatua ya ujumuishaji nchini Kenya na amechangia pakubwa katika usafishaji wa benki nchini Kenya,” imesema taarifa ya jarida hilo.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, benki ya Apex imesema kuwa ushindi huo ni mojawapo ya sifa za Bw Njoroge anazoendelea kupata hasa baada ya tuzo sawa na hiyo mnamo mwaka 2016.
Bw Njoroge alipokuwa akipokea tuzo hiyo alitambua juhudi za wafanyikazi wa CBK.
Alipokea tuzo hiyo Oktoba 20, 2019, jijini Washington D.C., Amerika katika hafla iliyofana.
Hii ni mara ya pili kwa Dkt Njoroge kupata tuzo hiyo, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2016 wakati alituzwa kutokana na juhudi zake za kupambana na mfumkobei.
Na katika tuzo yake ya mwaka 2019, ilitokana na uongozi wake wa kufanikisha shughuli ya kubadilishwa kwa noti za zamani za Sh1000 na noti mpya za thamani hiyo bila kuvuruga uthabiti katika soko la kifedha nchini, ilivyofanyika nchini India mnamo 2015.
Shughuli hiyo iliendeshwa kati ya Juni 1 na Septemba 2019 kikiwa ni kipindi cha miezi mitatu.
Dkt Njoroge, ambaye anahudumu kipindi chake cha pili kama Gavana wa CBK, alichangamkia tuzo hiyo huku akiwashukuru wafanyakazi wa taasisi kuwa kazi yao nzuri.
“Nafurahi na kuona fahari kuu kupokea tena tuzo ya Global Markets ya “Gavana Bora wa Benki Kuu katika Mataifa ya Kusini mwa Janga la Sahara Mwaka 2019. Nakushuru wafanyakazi wa CBK kwa kazi yao nzuri. Na naelekeza heshima ya tuzo hii kwa vijana wa Afrika,” akasema Njoroge katika ujumbe kwenye ukurasa wa akaunti ya Twitter ya CBK.
Alisema vijana ndio wanahitaji nafasi zaidi za kujiimarisha na “matendo yetu kama viongozi wa sasa yatatoa mwelekeo kwa manufaa yao.”
Dkt Njoroge anapata tuzo hiyo miezi mitatu pekee baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza kipindi chake cha kuhudumu kama Gavana wa CBK kwa miaka minne zaidi.
Hafla ya Tuzo ya Global Markets hufanyika kila mwaka wakati wa mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) jijini Washington D.C. ambako waunda sera wakuu hutambuliwa na kutuzwa.
Mnamo mwaka jana, 2018, Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria Godwin Emefiele alipata tuzo hiyo kwa kubuni njia endelevu za kudhibiti mfumkobei, kuimarisha uthabiti wa kiuchumi, kuimarisha imani ya wawekezaji na kuchochea kuimarika kwa upatikanaji wa mtaji kwa wafanyabiashara.
Dkt Njoroge ambaye aliteuliwa mnamo Juni 2015 ameweza kuhakikisha kuwa thamani ya shilingi ya Kenya inasalia katika wastani wa Sh102.97 kwa dola moja ya Amerika.
Vilevile, amedhibiti mfumkobei kusalia katika kiwango kinachokubalika na serikali na mashirika ya kimataifa ya kifedha.