Habari

Nyoro kuteua naibu wake ndani ya siku 14

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

GAVANA mpya wa Kiambu James Nyoro atalazimika kuteua naibu wake ndani ya kipindi cha siku 14 ijayo kulingana na ushauri uliotolewa na Mahakama ya Juu mnamo 2018.

Ushauri huo unawahitaji magavana kuwateua watu watakaoshikilia wadhifa wa Naibu Gavana ndani ya siku 14 ikiwa pengo litatokea na kuwasilisha jina la mteule huyo kwa Bunge la Kaunti ili achunguzwe kwa siku 60.

Bw Nyoro anaingia mamlakani Alhamisi; ikiwa ni muda wa saa chache baada ya Seneti kuidhinisha hoja ya kumwondoa mamlakani Waititu iliyopitishwa na Bunge la Kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 19, 2020.

Ushauri huo wa Mahakama ya Juu ulizingatiwa katika kaunti za Nyeri na Bomet pale manaibu wa magavana walipoingia afisini kufuatia vifo vya mabosi wao.

Katika Kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga ambaye alikuwa Naibu Gavana aliapishwa na kuanza kuhudumu baada ya kifo cha mkubwa wake Wahome Gakuru katika ajali ya barabarani.

Na kifo cha Joyce Laboso mnamo Juni 2019 kilitoa nafasi kwa naibu wake Hilarry Barchok kuingia afisini kama gavana.

Wawili hao, Kahiga na Bitok, wamewateua manaibu wao kwa mujibu wa ushauri wa Mahakama ya Juu, kutokana na upungufu katika Sheria ya Serikali za Kaunti na Katiba, kuhusu suala hilo.

Ni upungufu huo uliopelekea Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuamua kutoteua naibu wake zaidi ya miezi 18 baada ya kujiuzulu kwa Polycarp Igathe mnamo Januari 1, 2018.

Kufuatia uamuzi wa bunge la Seneti ulioofikiwa na maseneta 26 kati ya 38 waliopiga kura Jumatano usiku, Bw Ferdinand Waititu Babayao alikoma kuwa Gavana wa Kiambu kwa mujibi wa sehemu ya 33 (7) ya Sheria ya Serikali za Kaunti.

Bw Nyoro alichukua hatamu za uongozi wa kaunti hiyo rasmi kama gavana kwa mujibu wa kipengele cha 182 (2) cha Katiba na atahudumu kwa kipindi kilichosalia.

Ibara ya 3 (a) ya kipengele hicho inasema kuwa ikiwa wakati mtu anaingia afisini kama gavana zitakuwa zimesalia zaidi ya miaka miwili na nusu ya muhula mzima kabla ya uchaguzi mpya, itachukuliwa kuwa mtu huyo amehudumu muhula mzima.