Obama amtaja Raila kama shujaa wa demokrasia
ALIYEKUWA rais wa Amerika Barack Obama hatimaye aliandika ujumbe wa kumuomboleza aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Amolo Odinga aliyefariki dunia Oktoba 15 2025 akiwa na umri wa miaka 80, akipokea matibabu nchini India.
Ujumbe wa Obama ujiri baada ya presha kubwa kutoka kwa Wakenya mitandaoni, waliomkosoa kwa kukaa kimya kuhusu kifo cha mtu aliyekuwa na uhusiano wa karibu na familia yake na ambaye alitoka katika eneo ambalo linatambulika kama chimbuko la Obama, kaunti ya Siaya.
Kupitia akaunti yake rasmi ya X (zamani Twitter) mnamo Jumamosi, Oktoba 19 2025, Obama aliandika ujumbe wa kusisimua:
“Raila Odinga alikuwa shujaa wa kweli wa demokrasia. Alizaliwa wakati wa uhuru, na aliteseka kwa miongo kadhaa akipigania haki ya kujitawala na uhuru wa watu wa Kenya. Mara kwa mara nilimuona akiweka maslahi ya nchi mbele ya tamaa zake binafsi,” aliandika Obama.
Obama alimsifu Raila kama kiongozi wa maridhiano aliyeonyesha mfano wa msamaha bila kupoteza maadili yake ya msingi.
“Kama viongozi wachache sana duniani, alikuwa tayari kuchagua njia ya amani na maridhiano bila kuisaliti misimamo yake. Maisha ya Raila Odinga yalikuwa somo kwa Kenya na bara zima la Afrika, na dunia nzima. Nitamkosa sana,” alisema Rais huyo wa zamani.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Obama alituma rambirambi kwa familia ya Odinga na kwa watu wa Kenya, kwa niaba yake na mkewe, Mama Michelle Obama.
Hata hivyo, japo ujumbe huo ulipokewa kwa furaha na shukrani na wengi, ulijiri baada ya malalamishi mengi mitandaoni kutoka kwa Wakenya waliotaka Obama aonyeshe msimamo mapema, wakimkumbusha uhusiano wa muda mrefu aliokuwa nao na Raila na jamii ya Luo.
“Unamjua Baba? Raila Odinga? Huna la kusema?” aliandika wakili Cliff Ombeta (@OmbetaC) kwenye ukurasa wa Obama wa X wiki hii.
Obama na Raila wana historia na urafiki wa karibu wa kifamilia uliodumu kwa miaka mingi. Wote wawili wana asili Kaunti ya Siaya, na waliwahi kuonekana pamoja katika hafla kadhaa kabla na baada ya Obama kuwa Rais wa Amerika mwaka 2008.
Katika hotuba zake za awali, Obama amewahi kumtaja Raila kama ‘ishara ya matumaini kwa mustakabali wa kidemokrasia wa Afrika.”
Kifo cha Raila kimeendelea kuibua hisia kote duniani, huku viongozi kutoka mataifa mbalimbali wakimtambua kama mwanasiasa na mwanademokrasia asiye yumba na mwanaharakati aliyepigania haki, utawala bora na umoja
Obama, mmoja wa watu maarufu duniani, amejiunga na sauti nyingine kuu duniani kuenzi maisha na mchango wa Raila kwa Kenya na Afrika.