Habari

OCS ashtakiwa kutesa mwanamke aliyefika kituoni kulalamikia kunyanyaswa na polisi

Na RICHARD MUNGUTI April 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

AFISA mkuu wa polisi na mwenzake wa ngazi ya chini wameshtakiwa kwa kumtesa mwanamke aliyekuwa akifuatilia kesi ya kushambuliwa kwa kumweka kizuizini kinyume cha sheria kwa siku mbili katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga, jijini Nairobi, miaka minne iliyopita.

Bi Rebecca Njeri Muraya, ambaye ni Mkuu wa Kituo (OCS) cha Polisi cha Eastleigh North, na Sajenti Abdisalam Ahmed, walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Milimani, Lucas Onyina, ambapo walikana mashtaka ya kumtesa Ayni Hussein Mahammud mnamo Desemba 31, 2021.

Katika kesi hiyo, maafisa hao wawili wanashtakiwa kwa kumweka Ayni kizuizini kwa siku mbili kinyume cha sheria kama njia ya kumtisha ili aachane na kesi aliyokuwa ameanzisha dhidi ya Jama aliyedaiwa kumdhuru.

Bi Ayni alifika katika kituo cha polisi cha Eastleigh North kufuatilia hatua zilizochukuliwa dhidi ya Jama, ambaye inadaiwa alimshambulia Desemba 13, 2021. Badala ya kupata majibu, inadaiwa alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga ambako alizuiliwa kwa siku mbili.

Mbali na mashtaka ya kutesa, Muraya na Ahmed pia walikabiliwa na shtaka la matumizi mabaya ya mamlaka. Shtaka hilo linawahusisha moja kwa moja na tukio la kumkamata Ayni kinyume cha sheria katika kituo cha Eastleigh North na kumsafirisha hadi Muthaiga bila msingi halali wa kisheria.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), uliwasilisha ombi la kutaka wawili hao wasijibu mashtaka hadi baada ya siku saba wachambue faili mbili kutoka kwa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) na Kitengo cha Masuala ya Ndani cha Idara ya Polisi.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa vikali na wakili Simon Mburu anayemwakilisha Ayni. Wakili Mburu aliambia mahakama kuwa uamuzi wa kuwafungulia mashtaka Muraya na Ahmed uliafikiwa na DPP mnamo Januari 14, 2025, na jaribio la sasa la kutaka kuahirisha kusoma mashtaka ni ukiukaji wa utaratibu wa mahakama.

“DPP alipitia ushahidi uliowasilishwa na IPOA kabla ya kufanya uamuzi wa kuwafungulia mashtaka. Ombi jipya halina mashiko kisheria,” alisema Mburu.

Aliongeza kuwa karatasi ya mashtaka tayari imewasilishwa mahakamani na kwamba haki inahitaji washtakiwa wasomewe mashtaka yao. “DPP bado ana nafasi ya kuamua kuondoa au kufanyia marekebisho faili hata baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka,” alisisitiza.

Wakili wa utetezi, kwa upande mwingine, alisema hakuna tatizo la kisheria kwa DPP kuomba muda zaidi ili kupitia ushahidi uliokusanywa kutoka IPOA na Kitengo cha Masuala ya Ndani kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu kesi hiyo.

Katika uamuzi wake, Hakimu Onyina alieleza kuwa washtakiwa walitakiwa kufika mahakamani kusomewa mashtaka  Januari 23 2025 lakini hawakufika.

Tarehe nyingine ya Februari 13, 2025 pia ilipita bila kusomewa mashtaka kwa sababu za kiafya zilizotolewa.

Mahakama ilibaini Aprili 16, 2025, DPP aliomba tena muda wa siku saba kupitia faili la Kitengo cha Masuala ya Ndani.

Kwa kuzingatia usawa wa haki, Onyina aliamuru washtakiwa kusomewa mashtaka, lakini akaongeza kuwa DPP yuko huru kutumia muda wa siku saba alizoomba kufanya uamuzi wa kuendelea na kesi au la.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa Aprili 25, 2025.