Habari

ODM: Barua ya kujiuzulu kwa Gavana Orengo ni feki

Na CHARLES WASONGA August 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeitaja kama feki barua moja inayosambazwa mitandaoni na inayodai kuwa Gavana wa Siaya James Orengo amejiuzulu wadhifa huo.

“Tunasema kwamba barua iliyoandamanishwa ni FEKI. Ipuuze na UWE IMARA,” chama hicho kikasema Jumatatu, Agosti 4, 2025, kwenye ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa X.

ODM iliandamanisha barua hiyo na taarifa hiyo fupi.

Barua hiyo iliyodaiwa kuandikiwa Spika wa Bunge la Siaya George Okode, ilichipuza baada ya Gavana Orengo kukosa kuonekana hadharani tangu mapema mwezi Juni mwaka huu.

Hali hiyo imeibua wasiwasi na maswali miongoni mwa wakazi wa Siaya kiasi cha kumlazimu kiongozi wa ODM Raila Odinga kutoa hakikisho kuwa yu buheri wa afya.

Akiongea katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Ugenya Julai 27, 2025, Bw Odinga alisema “Orengo yu salama na atarejea afisini hivi karibuni.”

Bw Orengo alionekana hadharani kwa mara ya mwisho mnamo Juni 5, katika Ikulu ya Nairobi alipoongoza ujumbe wa viongozi wa Siaya kumtembelea Rais William Ruto.

Tangu wakati huo Gavana huyo wa Siaya hajaonekana hadharani.

Hata hivyo, jumbe zingali zinawekwa kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa X, kuhusu shughuli za kaunti na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mnamo Julai 25, Bw Orengo aliweka taarifa fupi akisema “Leo Betty (mkewe, Betty Murungi) na miye tulizuru boma la Bw na Bi K.V Rao.”

Taarifa hiyo iliandamanishwa na picha kadhaa.