HabariSiasa

ODM, Chap Chap wataka mageuzi ya mfumo wa utawala

February 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

VYAMA viwili vya kisiasa, jana viliwasilisha mapendekezo yake kwa Jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) jijini Nairobi, huku vikipendekeza mageuzi makubwa kwenye mfumo wa utawala nchini.

Chama cha ODM kilipendekeza kufutiliwa mbali kwa Wizara ya Ugatuzi, huku Maendeleo Chap Chap ikipendekeza kufutiliwa mbali kwa Seneti.

Akiwasilisha mapendekezo ya ODM, mwenyekiti wa chama hicho Bw John Mbadi alisema kuwa wizara hiyo imekosa kuoanisha utendakazi wa serikali hizo mbili kwa njia ifaayo, hali ambayo imekuwa ikizua matatizo ya mara kwa mara kama migomo ya wafanyakazi katika kaunti.

Alisema kuwa Mamlaka ya Mpito (TA), ambayo ilikuwa imepewa jukumu la kuhamisha baadhi ya majukumu ya Serikali ya Kitaifa kwa serikali za kaunti, haikufanikiwa kuweka utaratibu ambao ungezuia baadhi ya migongano ya kimajukumu ambayo imekuwa ikishuhudiwa.

“TA ilikosa kubaini wazi tofauti zilizopo kwenye baadhi ya majukumu ya serikali hizo mbili kama sekta ya kilimo, afya, ujenzi wa miundomsingi kati ya mengine. Hilo limekuwa likisababisha migomo ya mara kwa mara miongoni mwa wafanyakazi,” akasema Bw Mbadi, ambaye pia ni mbunge wa Suba Kusini.

Alisema kuwa majukumu hayo yanapaswa kukabidhiwa Kamati ya Kufanikisha Mahusiano kati ya Ngazi Mbili za Serikali (IGRC), kwa kuipa mamlaka zaidi kikatiba.

Naye Gavana Alfred Mutua wa Machakos, aliyewakilisha Maendeleo Chap Chap, alisema kuwa Seneti inapaswa kuondolewa, huku majukumu yake yakikabidhiwa Bunge la Kitaifa.

Alisema kuwa hadi sasa, Seneti haijaonyesha uzito wa majukumu ambayo imekuwa ikitekeleza ili kusimamia ugatuzi.

“Seneti ni kama mzigo kwa mlipaushuru. Inapaswa kufutiliwa mbali, kwani majukumu inayotekeleza yanaweza yakaendeshwa na wabunge,” akasema.

ODM pia ilipendekeza Kenya kuiga mfumo wa utawala wa Tanzania, ambapo Rais anachaguliwa moja kwa moja na wananchi. Chini ya mfumo huo, Rais humteua Waziri Mkuu kutoka chama ambacho kina wabunge wengi, ambapo baadaye huwa anaidhinishwa na Bunge.

Hata hivyo, kilipendekeza mamlaka ya Waziri Mkuu yawe wazi, ili kuepusha hali ambapo kuna mvutano wa kimamlaka kati ya viongozi hao wawili.

Hilo lilionekana kuondoa hofu, ambapo chama kimekuwa kikipendekeza uwepo wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka.

Dkt Mutua alipendekeza mfumo wa utawala, ambapo Rais, Naibu Rais, Waziri Mkuu na manaibu wake wawili wanachaguliwa pamoja.

Alisema kuwa hilo litaondoa hali ambapo utata utazuka, ikiwa Rais atakosa kuzingatia mikataba ya kisiasa wanayotia saini wakati wa kampeni.

“Tumeshuhudia hali ambapo mizozo ya kisiasa imeibuka baada ya viongozi kukosa kuzingatia mikataba wanayoweka. Ili kuepuka hilo, kuna umuhimu viongozi hao wote wachaguliwe moja kwa moja na wananchi, ili kusiwe na hali mizozo kama hiyo inaibuka,” akasema.

Baadhi ya mizozo kama hiyo ilishuhudiwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2002, ambapo Rais Mstaafu Mwai Kibaki alikosana na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga, kwa kutozingatia mwafaka waliotia saini baina yao.