ODM kusalia ndani ya Serikali hadi 2027
KATIBU Mkuu wa ODM Edwin Sifuna jana alionekana kunywea na kulegeza msimamo huku chama hicho kikiweka wazi kwamba kitaendelea kuwa ndani ya Serikali Jumuishi hadi mnamo 2027.
Akisoma taarifa ya Kamati Kuu ya ODM, Bw Sifuna ambaye amekuwa mkosoaji wa chama kuhusu ushirikiano wake na UDA, alisema kuwa hiyo ilikuwa nia na mapenzi ya Kinara wa taifa Raila Odinga.
“Tunasisitizia nia ya chama katika kusalia ndani ya Serikali Jumuishi hadi 2027, uhusiano ambao unaongozwa na ajenda 10 kwenye muafaka ulioafikiwa kuhakikisha kuna amani nchini,” akasema Bw Sifuna.
Kwa muda sasa, Seneta huyo wa Nairobi amekuwa mwiba kwa utawala wa Rais William Ruto huku akipinga mpango wowote wa kuunga kuchaguliwa kwake tena mnamo 2027.
Pia Bw Sifuna amekuwa akipinga Serikali Jumuishi, mara si moja akiikosoa kwa kutotekeleza yaliyomo katika muafaka wao uliotiwa saini na UDA na ODM baada ya maandamano ya Gen Z mwaka jana.
Kando na Sifuna, wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Babu Owino wa Embakasi Mashariki wamekuwa mstari wa mbele kupinga ushirikiano kati ya ODM na UDA.
Bw Sifuna alikariri kuwa chama hicho kitasalia imara hata baada ya mauti ya Raila Odinga akisema maoni kinzani ambayo yamekuwa yakishuhudiwa ni kawaida katika kudumisha demokrasia.
Mkutano wa jana ulikuwa wa kwanza wa ODM tangu Raila aage dunia mnamo Oktoba 16 na ulitumiwa kuidhinisha Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga kama kiongozi wa chama.
ODM pia ilitangaza kuwa kutakuwa na ibada sehemu mbalimbali ya kumuenzi Raila.
Hafla ya kwanza itaandaliwa eneobunge la Magarini Kaunti ya Kilifi mnamo Oktoba 2 na Oktoba 3.
Eneobunge hilo litakuwa na uchaguzi mdogo mnamo Novemba 27 ambapo mwaniaji wa ODM Harrison Kombe anaungwa mkono na UDA.
Ibada nyingine ya kumwomboleza Raila pia itaandaliwa Migori na Homa Bay mnamo Novemba 5 na 6 mtawalia.
Chama hicho pia kilithibitisha kuwa maadhimisho yake ya miaka 20 yataendelea jijini Mombasa jinsi yalivyopangwa.
Hafla hizo zitafanyika Novemba 14, 15 na 16 na zinalenga kuhakikisha kuwa kuna umoja chamani.
ODM ilisisitiza kuwa itaendelea kudumisha ndoto ya Raila huku pia ikitumia mkutano huo kutuma rambirambi kwa familia ya kigogo huyo wa siasa za upinzani.