ODM yayumba bila Raila wabunge wakipanga kuhama
WABUNGE kadhaa wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wamekiri wana mipango ya kuhama chama hicho na kuwania kwa tiketi ya vyama vingine vya kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Sababu kuu ya wabunge wengi kutaka kuondoka chama hicho kilicho na historia ya miaka 20, ni mkataba wa Serikali Jumuishi kati ya ODM na UDA, pamoja na mpango wa chama hicho kumsaidia Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027.
Wabunge wengine pia wameeleza hofu ya kutopata uteuzi wa chama, mabadiliko ya kisiasa, kuibuka kwa vyama vya kikanda vyenye mvuto, na kupungua kwa ushawishi wa ODM katika maeneo ya jadi kama Kisii na Magharibi.
Viongozi wanaoonekana kukosoa serikali jumuishi wanaogopa pia kutolewa kwa tiketi za chama kwa njia isiyo haki.
Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa atawania tena kupitia chama kipya mwaka 2027, huku Katibu Mkuu wa ODM na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, Seneta wa Kisii, Richard Onyonka, pamoja na wabunge Caleb Amisi (Saboti) na Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), wakisema watatafuta tiketi za vyama vingine iwapo ODM itasaidia Rais Ruto kupata muhula wa pili.
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ambaye anapanga kugombea kiti cha gavana wa Nairobi, na Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita, ambaye ameonyesha nia ya kumwondoa Gavana wa Migori, Ochilo Ayacko, wamesema wako tayari kuondoka ODM iwapo watashindwa kwenye mchujo.
Bw Omondi alisema kuwa uamuzi wake unachangiwa na historia ya ODM ya uteuzi usiokuwa wa haki na ukosefu wa viongozi thabiti baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, kiongozi na mwanzilishi wa chama.
Aliashiria pia jaribio la chama kumtimua ODM kwa kutembelea Rais Ruto Ikulu, jambo lililomfanya atishiwe na chama.
“Sitawania tiketi ya ODM. Nimekuwa nikifikiria hili kwa muda mrefu. Si nia yangu kutafuta tiketi ya ODM. Kwa kweli, nadhani nitawania kwa tiketi ya chama kingine. Ni chama gani na nitashirikiana na nani? Hayo tutaamua baadaye. Kile ni kipya kabisa,” alisema Bw Omondi.
Aliongeza kuwa alishinda uchaguzi wa 2022 kwa usaidizi wa Raila Odinga, lakini alikiri kuwa hofu ya kupoteza tiketi ilikuwa imemfanya afikirie kuwania kama mgombea huru.Mbunge Amisi alisema kuwa baadhi yao wanaweza kulengwa kwa kukosoa Serikali Jumuishi.
“Kama ODM itaamua kuunga mkono Ruto, sina chaguo ila kuondoka na kuwania kupitia chama kingine au kama mgombea huru,” alisema.
Bw Kibagendi naye alisema kuwa alijiunga na ODM kutokana na msimamo wake wa kulinda haki za binadamu, haki ya sheria na usawa wa rasilmali, lakini chama kimeachana na misimamo hiyo na sasa kinaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza, ambayo anasema inaendelea kukiuka haki za binadamu.
Seneta Onyonka aliwaonya viongozi wakuu wa ODM kuzingatia kuvunja uhusiano wao na UDA, akisema vinginevyo wabunge wengi watahama . Aliashiria kuwa serikali ya Kenya Kwanza imekosa kutekeleza ajenda ya vipengele 10, ambayo ndiyo msingi wa muungano kati ya ODM na UDA.
“Ninakusudia kugombea kupitia chama cha upinzani. Nitakuwa nje ya ODM ikiwa itaamua kumsaidia Ruto, kwa sababu Ruto hajafanya chochote kilichonifanya nifurahie kuwa katika serikali yake,” alisema Bw Onyonka.
Kadhalika, Bw Sifuna na wabunge wengine pia wameripotiwa kutafuta vyama vingine au kuwania kama wagombea huru.Mbali na hayo, Bw John Mbadi, Mwenyekiti wa ODM wa zamani aliyeteuliwa Waziri katika Serikali Jumuishi, alitaja hali hiyo kama mzozo wa kawaida unaotokea baada ya kifo cha kiongozi maarufu.